BALOZI wa Tanzania nchini Austria na Mwakilishi wa Kudumu wa Mashirika ya Kimataifa Vienna, Celestine Mushy, amefariki dunia katika ajali ya gari huku mwili wake ukiteketea kwa moto katika eneo la Mkata, mkoani Tanga.
Kutokana na kifo hicho, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi huku akieleza kuwa nchi imepata pigo kubwa.
Kwa mujibu wa ujumbe wa pole ulioandikwa kwenye akaunti ya Twitter, Rais Samia alisema taifa limeondokewa na mwanadiplomasia mahiri.
“Tumeondokewa na mwanadiplomaia mahiri na mtumishi makini wa umma. Mungu amweke mahali pema. Amina,” ilisema taarifa hiyo ya Rais.
Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Siriel Mchembe, aliiambia Nipashe kuwa Balozi Mushy alifariki dunia juzi kwa ajali ya gari eneo la Mkata akiwa njiani kwenda Moshi mkoani Kilimanjaro.
Alisema Balozi Mushy alikuwa anaendesha gari mwenyewe na alipata ajali baada ya kugongana na lori kisha likawaka moto.
“Hilo tukio lilitokea Jumanne usiku wakati akisafiri kuelekea Moshi. Aligongana na lori na magari yote yaliteketea kwa moto. Mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Handeni na taratibu zingine tunasubiri ndugu zake wafike kuutambua,” alisema Mchembe.
"Mwili wa balozi ulikutwa umeungua na tuliuchukua eneo la ajali usiku na tukaupeleka Hospitali ya Handeni. Ndugu zake wako njiani kutokea Dar es Salaam kwa ajili ya kuutambua na kuuchukua," aliongeza.
Akizungumza na Nipashe, mdogo wa Balozi Mushy, Ernest Mushi, ambaye alikuwa amefika katika hospitali ya Handeni kwa ajili ya utambuzi wa mwili alisema: “Sisi ndio tumefika hapa hospitalini. Bado tuko nje tunasubiri kuutambua mwili na baada ya hapo ndipo taratibu nyingine tutajua tunafanyaje.
“Lakini tumeambiwa kwamba alipata ajali baada ya kugongana na lori ambalo lilimfuata na alikuwa anaendesha gari mwenyewe,” alisema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Henry Mwaibambe, alisema ajali hiyo ilihusisha magari mawili, moja dogo aina ya Toyota Crown lenye namba ya usajili T 175 DMF mali ya Balozi Mushy ambalo lilikuwa linaendeshwa na mtu mmoja na liliungua hadi majivu.
“Ilikuwa ajali iliyohusisha magari mawili kugongana. Gari dogo aina ya Toyota Crown lilikuwa linaendeshwa na mtu mmoja na liliungua hadi majivu. Kwa hiyo tulikuwa kwenye utaratibu wa kupima mabaki ya mwili ili kujua kama kweli ni ya Balozi Mushy kutokana na kuungua sana kiasi cha kutokutambulika kwa macho,” alisema Kamanda Mwaibambe.
“Baadhi ya ndugu wa Balozi walikuja. Kwenye usajili wa gari, jina lake linaonyesha ni lake hiyo ndiyo maana wanahisi ni yeye. Tunasubiri uchunguzi wa wataalam ufanyike kwa haraka tutajua tu,” alisisitiza Kamanda Mwaibambe.
Balozi Mushy aliteuliwa na Rais Samia kushika nafasi hiyo Januari, mwaka huu, na Mei aliwasilisha Hati ya Utambulisho kwa Rais wa Jamhuri ya Austria, Alexander Van Der Bellen.