Mjane wa Mengi agonga mwamba kesi ya mirathi




Dar es Salaam. Mjane wa aliyekuwa mfanyabiashara maarufu nchini, Reginald Mengi, Jacquiline Ntuyabaliwe na wanawe, wamekwama kutetea wosia ulioachwa na marehemu baada ya Mahakama ya Rufani kutupa shauri lake la kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu.

Jacquiline alifungua shauri mahakamani hapo la mapitio kufuatia hukumu ya Mahakama Kuu, iliyokataa wosia uliodaiwa kuachwa na Mengi.

Shauri hilo la mirathi namba 39 ya mwaka 2019, lilifunguliwa na watu wanne, wakiwemo ndugu wa marehemu Mengi.

Mahakama hiyo katika uamuzi wake uliotolewa juzi na jopo la majaji watatu, Rehema Mkuye (kiongozi), Dk Paul Kihwelu na Panterine Kente lilitupa shauri hilo kutokana na kasoro mbili zilizoonekana kwenye kiapo cha Jacquiline na cha wakili wake, Audax Kahendaguza vilivyoambatanishwa katika maombi hayo.


Kasoro hizo ambazo mahakama imekubaliana nazo ni viapo kuwa na maelezo yasiyopaswa kuwemo kwa hoja zinazohitaji ushahidi, maoni, mapendekezo na hitimisho na nyingine ni kutokubainisha chanzo cha taarifa ziliozokuwemo kwenye viapo hivyo.

Mahakama hiyo ilifikia uamuzi huo kutokana na pingamizi la awali lililowekwa na wasimamizi wa mirathi hiyo walioteuliwa na Mahakama Kuu ambao ni Abdiel Reginald Mengi akishirikiana na mdogo wake marehemu Mengi, Benjamin Abrahamu Mengi, kupitia kwa mawakili wao, Michael Ngalo na Roman Masumbuko.

Katika uamuzi huo, mahakama imesema kiapo kinapokuwa na kasoro kama hizo, aya zenye kasoro huondolewa kwenye kiapo na kuendelea na aya nyingine zisizo na kasoro.


Hata hivyo, imesema aya zenye kasoro ndizo msingi wa shauri hilo na kwamba, baada ya kuziondoa zinazobaki haziwezi kusimama zenyewe.

“Kasoro hizo zinayafanya maombi haya kutoweza kusimama, hivyo tunayatupilia mbali. Kwa kuwa shauri linatokana na mirathi hatutoi amri yoyote kuhusu gharama,” imesema mahakama hiyo katika uamuzi huo.

Awali, watu wanne, Benson Benjamini Mengi, William Onesmo Mushi, Zoebu Hassuji na Sylvia Novatus Mushi walifungua shauri la msingi la mirathi Mahakama Kuu wakiomba kuteuliwa kuwa wasimamizi wa mirathi hiyo, kwa mujibu wa wosia ulioachwa na Mengi.

Hata hivyo, Abdiel na Benjamini waliweka pingamizi dhidi ya wosia huo unaompa Jacquiline na wanawe haki ya urithi wa mali za Mengi, wakipinga uhalali wake huku wakiwasilisha jumla ya sababu nne za kuupinga.


Mahakama Kuu baada ya kusikiliza hoja za pande zote ilikubaliana na hoja za pingamizi dhidi ya wosia huo na kuikataa kuwa ni batili.

Jaji Yose Mlyambina alikubaliana na sababu hizo za pingamizi huku akisema unawanyima urithi wanawe wengine (wakubwa, Abdiel na ndugu yake) bila kutoa sababu.

Pia Jaji Mlyambina katika hukumu yake hiyo ya Machi 18, 2021, aliukataa wosia huo akieleza kuwa ziliiingizwa mali za mke wake mkubwa na kwamba nakala yake alikuwa nayo mwenyewe Jacguiline Mengi ambaye alikuwa mnufaika.

Hivyo Jaji Mlyambina aliwateua Abdiel na Benjamini kuwa wasimamizi wa mirathi na akaelekeza mali za marehemu zigawiwe warithi wanaostahili kwa utaratibu wa kawaida kama wa mtu ambaye hakuacha wosia.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad