PAROKO wa Parokia ya Haydom kanisa katoliki Jimbo la Mbulu mkoani Manyara, Padri Baltazar Sulle (63), amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara, mjini hapo, akikabiliwa na madai ya wizi wa Sh. milioni 20 za kaka yake.
Padri Baltazar anadaiwa kuchota fedha hizo kwenye akaunti ya kaka yake, aitwaye Dionis Margwe.
Akisoma hati ya mashtaka inayomkabili Paroko huyo, Wakili wa Serikali, ambaye aligoma jina lake lisichapishwe gazetini, alidai kwamba wizi huo ulifanywa na paroko huyo pamoja na wafanyakazi wawili wa Benki ya NMB.
Aliwajata wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni wafanyakazi wa Benki ya NMB, Cynthia Nyamtiga (27) na Winfrida Rwakilomba (30).
Kesi hiyo namba 44 ya mwaka huu inasikilizwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi, Mariam Lusewa.
Katika hati ya mashtaka, mshtakiwa wa kwanza, Padri Baltazar anadaiwa kuiba fedha hizo ambazo zilitokana na mirathi ya shemeji yake na kaka yake ambaye alishafariki dunia.
Iliendelea kudaiwa mahakamani hapo kuwa, Paroko Sulle, alitenda kosa hilo Machi 3, mwaka 2021.
Anadaiwa kutenda kosa la kwanza ambalo ni wizi kinyume na kifungu cha 258 (1) na kifungu cha 265 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 ya Sheria iliyofanyiwa Marejeo Mwaka 2022.
Shtaka la pili linalomkabili Padri Sulle, ni kugushi nyaraka kinyume na kifungu cha 333 na kifungu cha 355 (a) na kifungu cha 335 (d) (i) wakati shtaka la tatu linawakabili washtakiwa wote watatu.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Hakimu Lusewa alitoa masharti ya dhamana na washtakiwa wote watatu walitimiza vigezo na kuachiwa kwa dhamana ya bondi ya Sh. milioni saba kwa kila mdhamini.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba 21, mwaka huu, itakapotajwa tena.