Phiri asimulia alivyoitosa Yanga, asema yupo Simba kimkakati



KINARA wa mabao Simba anayeongoza pia orodha ya wafungaji wa Ligi Kuu sambamba na Fiston Mayele, Mzambia Moses Phiri amefichua siri nzito aliyokaa nayo tangu atue nchini kukipiga Msimbazi.

Phiri mwenye mabao ameweka bayana namna alivyofuatwa na klabu tatu kubwa nchini, Yanga, Azam na Simba na kuamua kutua Msimbazi kutokana na mmoja wa vigogo wa klabu hiyo kumfuata na kumwambia ‘chonde chonde’ asiende kokote na badala yake atua timu hiyo kwa jinsi walivyomhitaji.

Akizungumza na Mwanaspoti katika mahojiano maalum akitoka kutupia mabao mawili wakati Simba ikiizamisha Coastal Union kwa mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga, Phiri alisema kabla ya kufanya maamuzi ya kujiunga Simba tayari Azam na Yanga zilikuwa zikimfukuzia.

Alisema Azam viongozi wake wawili walikuwa wakimpigia simu kila siku ili kumsihi aende Chamazi, lakini Rais wa sasa wa Yanga, Injinia Hersi Said alimfuta kabisa Zambia na kuzungumza naye, lakini mabosi wa Simba walivyosikia amefuatwa na wapinzani wao walimfungia kazi ki kwelikweli.


“Yanga ilionyesha dhamira ya kunichukua na kiongozi wao alinifuata kabisa Zambia, lakini Simba ilimtumia mmoja wa vigogo (jina tumelihifadhi) na kunisihi nisiende Yanga wala Azam, kwani walikuwa wakinihitaji, alisema Phiri na kuongeza;

“Kigogo huyo aliniambia wapo tayari kunipa chochote ili nitue Msimbzi kwani walikuwa wakinihitaji mno kwa kumueleza washambuliaji wake (kipindi hicho), John Bocco, Meddie Kagere na Chriss Mugalu walichemsha licha ya msimu wa nyuma kufanya vyema. Tena wanitaka nijiunge dirisha dogo.”

Phiri anayemiliki mabao matano katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua za awali yaliyoiwezesha Simba kutinga makundi, alisema yupo timu hiyo kimkakati kwa kazi maalumu.


“Kwa heshima iliyonipa Simba sikuona sababu ya kuhangaika na wengine, ndio maana nikaipotezea Yanga na Azam na kuamua kutua Msimbazi.”

“Nakumbuka nilimjibu kiongozi huyo naweza kufanya kazi hiyo ya kufunga bila shida yoyote nikishirikiana na wachezaji wenzangu naimani kubwa kufanya vizuri ndani ya mzunguko wa kwanza,” alisema Phiri na kuongeza;

“Baada ya kufika nchini kujiunga na Simba viongozi wa juu, Salim Abdallah na Barbara Gonzalez kila mmoja kwa nafasi yake aliniambia wana imani kubwa nami na kufanya vizuri kama ilivyokuwa Zambia. “Basi baada ya kupatiwa kila nilichokuwa nahitaji kwenye mkataba wangu deni kubwa lilibaki kwangu kutimiza yale makubaliano yetu na viongozi hao pamoja na imani kubwa waliyoiweka kwangu.”

Kuhusu kasi yake ya mabao kwa sasa alisema; “Nashukuru Mungu ndani ya duru la kwanza licha ya kukosa baadhi ya mechi kwa kushirikiana na wachezaji wenzangu nimeweza kufanya lile ambalo nilikuwa naimani naenda kulitimiza.”


“Simba kuna wachezaji wengi wazuri kwa kushirikiana na wao katika duru la pili naweza kufunga zaidi ya haya mabao niliyofunga sasa kwenye ligi na nikaendelea makali hadi kwenye hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika,” alisema Phiri ambaye msimu uliopita akiwa na Zanaco alifunga mabao 14 katika Ligi Kuu ya Zambia.

Kuhusu kuchukua tuzo za Mfungaji bora, alisema anatamani ila hilo ni kipaumbele chake cha pili baada ya kile ya kuiwezesha Simba kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad