Rais Samia atia neno sakata la mabehewa




Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ameingilia kati sakata la mabehewa lililoibua gumzo kwenye mitandao ya jamii na vyombo vya habari, akisema hata kama mabehewa yalishatumika, basi yamekarabatiwa vizuri kutoa huduma.

Hivi karibuni, Serikali imenunua mabehewa 39 ambapo kati yake 14 ni ya reli ya kisasa (SGR) na mengine 22 ni ya reli ya kawaida.

Akizungumza leo Desemba 20 kwenye hafla ya kutia saini wa mkataba wa ujenzi wa awamu ya pili ya reli ya kisasa (SGR) kwa kipande cha Tabora hadi Kigoma, amesema yeye mwenyewe ameyashuhudia mabehewa yaliyonunuliwa na Serikali akisema yamekarabatiwa vizuri.

“Nilishawahi kupanda treni kwenda mikoa ya katikati na niliwekwa daraja la kwanza na daraja la kwanza, daraja hilo sio hata la treni ile.


“Kwa hiyo tunakotoka ndugu zangu ni mbali na lazima tushukuru,” amesema.

Huku akiwaonya watu wanaokosoa mabehewa hayo, Rais Samia amesema baadhi ya watu hawajui nchi ilipotoka.

“Anayefuja mwenyewe kazaliwa miaka 1990 na hajui tunakotoka anajua tulipo anakufananisha na Ulaya na Marekani anakokuona na anataka Tanzania ifike kule bila kujua hata wale anaowafananisha nasi nao wanamiaka zaidi ya 200 ya maendeleo hadi kufika pale na Tanzania tuko mwaka wa 60,” amesema.


Amesema Watanzania wanapaswa kushukuru na Serikali anayoiongoza itaendelea kufanya mambo mazuri huku akieleza kabla ya kuja kwenye hafla hiyo alikuwa ananog’ona na Katibu mkuu kuhusu mabehewa hayo.

“Tukasema hawa hawajui wamezaliwa Dar wamekulia Dar sisi Waha tulikulia Kigoma tuliokuja huku tunajua kuna kitu serikali imefanya kwa hiyo wale ambao hawayagusi wataona jambo dogo, lakini kwa wale wanaoguswa na hayo maendeleo ni jambo kubwa sana,” amesema.

Miongoni mwa watu waliokosoa ubora wa mabehewa yaliyonunuliwa na Serikali ni Mbunge wa Nzega Vijijini Dk Hamis Kigwangalla aliyedai kuwa na taarifa za ununuzi wake.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa Shrika la Reli (TRC), Masanja Kadogosa aliwataka Watanzania kupuuza madai ya wakosoaji wa mabehewa hayo.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad