LICHA ya kuwepo kwa tafiti mbalimbali zilizofanywa na Taasisi ya Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na tafiti zilizofanywa na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) katika kutekeleza miradi yake na kuangala hali halisi ya rushwa ya ngono nchini hususan katika maeneo ya makazini, vyumba vya habari pamoja na vyuo vikuu, bado kuna uhitaji wa tatizo hili kuendelea kupigiwa kelele kutokana na jinsi lilivyoshamiri.
Kuna athari kubwa kwa jamii katika rushwa ya ngono na unyanyasaji wa kingono kwani huwafanya mabinti wengi kurudi nyuma kimaendeleo na kimasomo pindi wanapokutana na madhila hayo.
Hivi karibuni, akifungua Kongamano la Wadau wa Rushwa ya Ngono kwa Wanafunzi na Wakufunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Naibu Waziri Utumishi, Deogratius Ndejembi, amesema rushwa ya ngono inasababisha kuzalishwa wasomi wasio na tija na kuwanyima haki wanafunzi.
Kauli hiyo ya Waziri Ndejembi, inachochea mjadala unaoonyesha zaidi ukubwa wa tatizo hili na kutukumbusha Watanzania kuchukua hatua za ziada kupambana na rushwa ya ngono mashuleni, vyuoni na katika sekta ya ajira na utumishi wa umma, tatizo ambalo linatishia kuharibu vipaji.
“Huu ni wakati sasa kwa wadau wanaopinga ukatili wa kijinsia, watetezi wa haki za binadamu, wahanga wa ukatili na serikali kukumbushana kuwa rushwa hii inavunja haki za binadamu, ni kosa la jinai kisheria, inaharibu utu na inaua vipaji hapa nchini,” anasema Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Dk. Rose Reuben alipozungumza katika maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia yaliyofanyika Novemba 29, 2022 jijini Dar es Salaam.
Anasema TAMWA katika utafiti wake wa mwaka 2021 kwa kushirikiana na Mfuko wa Udhamini wa Wanawake (WFT-T) iligundua tatizo la rushwa ya ngono limeathiri mfumo mzima wa vyombo vya habari kuanzia vyuo vya uandishi hadi ndani ya vyombo vya habari,” anasema.
“Mbali na rushwa hiyo kuwakumba wasomi, kuna changamoto ya wanahabari wanawake kuacha kazi juu ya kadhia hiyo, huku wapo wanafunzi walioacha kusoma uandishi wa habari kuhofia janga hilo,” amesema.
Dkt. Reuben anasema katika tafiti waliyoifanya waliweza kubaini kuwa tatizo kubwa la rushwa ya ngono na unyanyasaji wa kingono mahala pa kazi na katika elimu ya vyuo vikuu.
“Matokeo ya tafiti na uchapishaji wa habari kuhusu rushwa ya ngono, yalichagiza wadau na waathirika kuweka wazi hali halisi ya rushwa ya ngono na unyanyasaji wa kingono katika mazingira ya kazi na elimu,” anasema na kuongeza.
“Katika utafiti huo, pia TAMWA imebaini asilimia 48 tu ya wanahabari ndiyo wanaoweza kusema wazi kuhusu madhila ya rushwa ya ngono wanayopitia katika vyumba vya habari huku asilimia 52 inayobaki, hawawezi kusema wazi kuhusu changamoto hiyo,” anasema na kuongeza.
“Kila mmoja katika majukumu yake anapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha rushwa ya ngono haiathiri mfumo wa elimu wala kazi,” anasema.
Dkt. Reuben anasema kwa mujibu wa Kifungu cha 25 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11/ 2007, mtu yeyote ambaye kwa kutumia nafasi yake au mamlaka yake katika kutekeleza majukumu yake anaomba au kutoa upendeleo wa kingono au upendeleo mwingine wowote kama kigezo cha kutoa ajira, kupandishwa cheo, kutoa haki au upendeleo wowote unaotambulika kisheria, atakuwa ametenda kosa chini ya kifungu hiki.
Aidha anasema utafiti uliofanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mwaka 2020 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Utumishi, Deogratius Ndejembi, anasema rushwa ya ngono inasababisha kuzalishwa wasomi wasio na tija na kuwanyima haki wanafunzi.
Nae Mwenyekiti wa Mtandao wa Kupambana na Vitendo vya Ukatili wa kijinsia (MKUKI) Wakili Anna Kulaya anasema serikali iharakishe kuridhia mkataba wa kimataifa unaopinga rushwa ya ngono mahala pa kazi kwa kuwa utasaidia kuweka msimamo wa serikali dhidi ya vitendo hivyo na kufikia ziro ifikapo 2030. “Tunaiomba Serikali kuharakisha kuridhia mkataba wa C190, hii itasaidia katika kupambana na vitendo vya Rushwa ya Ngono na Unyanyasaji mahala pa kazi,anasema Wakili Kulaya
Anasema watu wote wanawajibu wa kuwa mstari wa mbele na kuhakikisha tunapinga vitendo vya Rushwa ya Ngono vyuoni na mahala pa kazi.”Wapo viongozi katika maeneo ya kazi, wanaotoa kazi kwa upendeleo kwa kuomba rushwa ya ngono badala ya kuangalia uwezo na vipaji.”anasema
Naye Mmoja wa Wakilishi wa Mtandao wa ushirikishwaji Wanaume (MET), Dk. Lazarus Katanta anasema wanaume nao hawana budi kuwemo katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia kwakuwa wao ndio watuhumiwa zaidi wa vitendo hivyo.
“Wanaume tunapaswa kujua rushwa ya ngono inaua ndoto za wanawake wengi, hebu kazi yetu tujikite hasa katika kukagua vyeti na sio maungo,” anasema
Dkt. Katanta anasema kwa kuiomba serikali kuridhia mkataba huo ili kuondoa kadhia hiyo ya rushwa ya ngono ambayo imekuwa ikiwatesa wanawake wengi hasa mahala pa kazi.
Naye mwanafunzi wa Chuo kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT),Teresia John ambaye anasema “kwa upande mwingne sisi wasichana tuna katabia cha kuwatega wahadhiri ili tu kupata alama nzuri kitendo ambacho ndicho kinazidi kuchochea rushwa hiyo ndani ya taasisi za kielimu, hivyo tukianza sisi wanafunzi kuacha tabia hiyo naimani kwamba hata wanaotupigania,”anasema na kuongeza
“Sisi wanafunzi tuzingatie kujithamini kuwajibika na kujitambua pamoja na kwamba mwalimu atataka kukurudisha nyuma kimasomo kama umewajibika na kusoma ipasavyo utakuwa na jeuri ya ufaulu wako katika mitihani” anasema Anna Hangwa Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tumaini jijini Dar Es Salaam