MABOSI wa Simba wajanja sana, kwani baada ya kusikia kocha msaidizi aliyekuwa masomoni, Seleman Matola anatakiwa na klabu moja ya Ligi Kuu Bara, fasta wakaamua kufanya mambo kwa kumpandisha cheo ili aendelee kusalia klabuni, huku mwenyewe akifunguka kila kitu juu ya ishu hiyo.
Matola amerejea hivi karibuni kutoka kwenye kozi ya ukocha wa Leseni A ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), iliyofanyika visiwani Zanzibar na taarifa kutoka ndani ya Simba zinasema huenda akabadilishiwa majukumu kwenye kikosi hicho.
Taarifa hizo zinasema Matola atabadilishiwa majukumu kwa kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa klabu hiyo na kusimamia makocha wote.
Mchakato huo wa Matola kubadilishiwa majukumu ya kuwa Mkurugenzi wa Ufundi upo hatua ya mwisho na hii imekuja baada ya kupata fununu ya kuwa na dili nono la kutakiwa na klabu ya Namungo iliyotangaza Denis Kitambi kuwa kocha msaidizi.
Awali, Matola kabla ya kwenda kusoma alikuwa akifanya kazi chini ya Juma Mgunda na kama mchakato huu wa sasa utakamilika maana yake atakwenda kuwa bosi wa juu ndani ya kikosi hicho chini ya makocha wote.
Majukumu ya cheo hicho kipya ni pamoja na kusimamia timu kubwa, timu za vijana zilizokuwa chini ya kocha, Mussa Mgosi anayefanya kazi na Mgunda katika timu kubwa kwa sasa pamoja na timu ya wanawake iliyopo chini ya kocha, Charles Lukula.
Mabosi wa Simba hata kama wakimaliza mchakato wao wa kuleta kocha mkuu wa kigeni atafanya kazi zote za ufundi ndani ya kikosi hicho na mwisho wa siku atakuwa anaripoti kwa Matola kwani ndiye bosi wake.
Katika kuhakikisha jambo hili linakamilika ili Matola aweze kukubaliana nalo tangu aliporejea kutokea Zanzibar amekuwa akifanya vikao vya mara kwa mara na viongozi ili kulikamilisha mapema, huku ikielezwa tayari klabu kadhaa zilikuwa zikitaka huduma ya Matola ikiwamo Namungo.
Awali, alihusishwa na Polisi Tanzania aliyowahi kuinoa kabla ya kurejeshwa Msimbazi na kama mabosi watashindwa kukamilisha dili la kumpa cheo kipya haitashangaza kuona Matola akienda Namungo kuchukua nafasi ya Hanour Janza, kutoka Zambia ambaye haonekani kwa sasa kwenye timu hiyo ambayo juzi usiku ilikubali kipigo cha kwanza nyumbani kutoka kwa Yanga ikifungwa 2-0.
Matola kama atakubali dili hilo la Namungo lenye mpunga mrefu atakwenda kuwa kocha mkuu huku chini yake kukiwa na makocha wengine wawili wasaidizi, Shedrack Nsajigwa na Denis Kitambi.
Alipotafutwa na Mwanaspoti, alijibu kwa kifupi kwamba hakuwa kwenye nafasi ya kufafanua lolote.