MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imeeleza wahalifu wa mitandao ya simu maarufu kama 'Tuma kwa namba hii' wanavyosajili laini kinyemela kwa kutumia vitambulisho na alama za vidole vya watu, bila wahusika kugundua.
Imesema uhalifu huo hufanywa na mawakala wanaosajili laini za simu mteja anapokwenda kujisajili akiwa na kitambulisho kwa kumtaka kuweka alama za vidole kwenye mashine zaidi ya mara moja kwa kisingizio alama haijasoma.
Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Bidhaa za Mawasiliano TCRA, Thadayo Ringo, alibainisha udanganyifu huo juzi wakati akitoa mafunzo ya kuzijengea uwezo wa kukabiliana na makosa ya mitandaoni Kamati za Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano za mikoa kupitia Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA- CCC).
"Ukienda kusajili laini ukiona umechukuliwa alama za vidole, akaendelea kuingiza taarifa akarudi kukuambia tena alama hazijakubali rudia tena usikubali, anatumia taarifa zako kusajili laini zaidi ya moja na kuwapatia wahalifu," alisema Thadayo.
Alisema wahalifu wa mitandao wamekuwa wakiibuka na mbinu mpya kila mara na TCRA huchunguza na kuzibaini kuhakikisha wanadhibiti uhalifu.
Maelezo hayo yalitokana na swali lililoulizwa na mmoja wa wajumbe hao, Ally Nassoro
kutoka Tanga, aliyetaka kufahamu TCRA inashindwaje kuwakamata wahalifu wanaotumia simu zilizosajiliwa kuomba fedha kwa watu.
Alisema ili kumaliza tatizo hilo, kila mtumiaji wa laini ya simu anatakiwa kupiga namba *106# kutazama idadi ya namba za simu zilizosajiliwa kwa namba yake ya Kitambulisho cha Taifa kinachotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
Alisema baada ya kupiga namba *106# utapewa chaguzi kadhaa namba 1 hadi 5, ukichagua namba 3 utatazama idadi ya namba za simu zilizosajiliwa kwa namba yako ya uraia iliyotolewa na NIDA.
Kwa mujibu wa Thadayo, mtumiaji wa huduma za mawasiliano ya simu za mkononi akibaini namba za ziada, zaidi ya zilizosajiliwa kwa namba yake ya NIDA, atatakiwa kuchukua hatua ya kufika katika dawati la huduma kwa wateja ili kutoa taarifa itakayowezesha kufutwa kwa namba ambazo hakuzitambua.
Alisema hatua hiyo ni muhimu kwa kuwa inamlinda mtumiaji wa huduma za mawasiliano dhidi ya matumizi mabaya ya namba hizo yakiwamo yanayohusisha uhalifu.
Alisema mwakani wataanza kuzifungia lakini zote zisizohakikiwa na zinazomilikiwa nyingi na mtu mmoja.