Tuhuma za Ramaphosa zawagawa Afrika Kusini



Johannesburg. Mustakabali wa kisiasa wa Rais Cyril Ramaphosa uko shakani baada ya kuibuka tuhuma za kuficha fedha katika shamba lake, huku wananchi wakijiuliza atajiuzulu au ataendelea kubakia madarakani?

Juzi kulikuwa na tetesi za kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 70 kuwa anatarajia kujiuzulu baada ya kuongezeka shinikizo la kumtaka afanye hivyo, lakini hadi jana asubuhi hakufanya hivyo.

Taarifa kutoka kwa watu walio karibu na Rais Ramaphosa wanadai kuwa wamemshauri apambane kusafisha jina lake na kuueleza umma ukweli.

Taswira na kupanda kwake kisiasa kulichagizwa zaidi kutokana na vita vyake dhidi ya ufisadi uliotawala Chama cha African National Congress (ANC) na nchi hiyo iliyokuwa iikiongozwa na Jacob Zuma.


ANC ni chama kinachotawala Afrika Kusini tangu mwisho wa ubaguzi wa rangi mwaka 1994, kilipaswa kufanya kikao cha dharura cha kujadili mgogoro uliozidisha migawanyiko ya vyama.

Ramaphosa amekuwa akishutumiwa tangu Juni, mwaka huu, wakati mkuu wa zamani wa makachero alipowasilisha malalamiko polisi akidai kuwa alificha wizi wa pesa taslimu katika shamba lake la Phala Phala Kaskazini Mashariki mwa Afrika Kusini.

Ripoti mbaya kutoka kwa jopo la wataalamu wa sheria linadai Rais Ramaphosa alificha wizi wa Dola milioni 4 (zaidi ya Sh bilioni 8).


Jopo hilo linaloongozwa na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu – liliezea baadhi ya maelezo yake ‘sio ya kweli’. Wakosoaji wake wanasema si tu kwamba Ramaphosa ana kesi ya kujibu mbele ya Bunge, bali pia kwa raia wa Afrika Kusini.

Kwa kuzingatia misimamo mikali ya vyama vya upinzani ambavyo baadhi yao vinamtaka aachie ngazi mara moja, kashfa hiyo inaweza kumgharimu kazi yake.

Utetezi wa Ramaphosa

Katika wasilisho la kurasa 138 kwa jopo hilo, Rais Ramaphosa alikanusha kuwa kulikuwa na kitu kibaya kuhusu pesa zilizofichwa kwenye shamba lake binafsi, akisema zilitokana na mapato ya nyati waliouzwa kwa Dola 580,000 (zaidi ya Sh1.2 bilioni) kwa raia wa Sudan, Mustafa Mohamed Ibrahim Hazim, mwishoni mwa 2019.

Hata hivyo, Hazim hajajitokeza hadharani kueleza kwa kina tuhuma hizo na mambo yake mengi hayajulikani.


Jopo hilo lilihoji kwa nini stakabadhi iliyowasilishwa kwao haikuwa na maelezo yoyote ambayo yangemfanya atambulike. Kulikuwa na jina lake tu, hakuna anwani ya biashara wala nambari ya kitambulisho.

“Kwa heshima nasema mashtaka yote niliyoitwa kuyajibu hayana msingi wowote, madai mengi yalikuwa uvumi na ninaomba suala hilo lisiendelezwe,” alisema Rais Ramaphosa katika utetezi wake.

Katika maelezo ya Rais Ramaphosa, meneja wa nyumba ya kulala wageni katika shamba hilo alihifadhi kwanza pesa hizo kwenye sefu, lakini baadaye akazihamishia kwenye sofa katika chumba cha kulala cha ziada “ndani ya makazi yangu ya kibinafsi, kwa sababu alidhani kuwa ni mahali salama zaidi, kwani aliamini hakuna mtu angevunja na kuingia katika nyumba ya Rais.”

Hata hivyo, jopo la kuchunguza tuhuma hizo limeweka wazi kuwa maelezo ya Rais yanahitaji kuchunguzwa ili majibu ya kwa nini alihifadhi Dola 580,000 ndani ya sofa? Kwa nini wizi wa fedha hizo haukuripotiwa polisi miaka miwili iliyopita? Kwa nini nyati anaosema waliuzwa bado wamebaki shambani yapate majibu.


Chama cha Democratic Alliance cha Afrika Kusini, kilitangaza kwamba kitatumia kikao cha bunge wiki ijayo kuwasilisha hoja ya kutaka uchaguzi wa mapema, kikisema shutuma dhidi ya Rais Ramaphosa zinaonyesha kwamba ANC lazima iondolewe madarakani.

“Ripoti iko wazi na haina utata. Kuna uwezekano mkubwa Rais Ramaphosa alikiuka vifungu kadhaa vya Katiba na ana kesi ya kujibu. Taratibu za kumfungulia mashtaka lazima ziendelee,” kilisema.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad