Mfanyabiashara anayemiliki Mabasi ya Shabiby, Ahmedy Shabiby ambaye pia ni Mbunge wa Gairo amesema alifanikiwa kununua Basi lake la kwanza akiwa na umri wa miaka 19 kutokana na kufanya kazi kwa bidii na kusisitiza kuwa hakuna mbadala mwingine wa mafanikio zaidi ya kufanya kazi kwa bidii.
Mbunge Shabiby ameyasema hayo kwenye Kongamano lililoandaliwa na Umoja wa Vijana wa CCM Wilaya ya Gairo kwa ajili ya kumpongeza mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Dr Samia Suluhu Hassan kwa kuchagulia kuwa mwenyekiti wa chama hicho na kumpongeza Mbunge huyo kwa kutimiza miaka 17 ya Ubunge katika Jimbo la Gairo.
Shabiby amesema wakati anasoma alikuwa akijishughulisha na biashara ndogondogo na kilimo jambo lililomfanya akiwa na umri wa miaka 19 aweze kununua basi lake la kwanza la kusafirisha abiria.
Shabiby ameongeza kuwa Watu wengi wamekuwa wakidhani mafanikio aliyoyapata yametokana na kuzaliwa kwenye familia ya kitajiri na kurithi mali jambo ambalo amesema sio la kweli bali siri ni kufanya kazi kwa kujituma na kwa bidii bila kukata tamaa.