Vitambulisho Nida kupatikana kwa njia ya mtandao




Dar es Salaam. Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imetambulisha mfumo wa usajili wa watu kwa njia ya mtandao utakaowezesha wananchi wenye sifa za kuomba vitambulisho vya taifa kwa kujaza fomu mtandaoni.

Waombaji wa awali watajaza fomu mahali popote walipo bila kulazimika kwenda ofisi za usajili za wilaya au vituo vya usajili vya Nida kupitia tovuti eonline.nida.go.tz katika mtandao na kufuata malekezo.

Hayo yamesemwa leo Jumatano Desemba 21, 2022 na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha NIDA, Geofrey Tengeneza wakati wa kutambulisha mfumo huo mpya kwa waandishi wa habari.

Amesema mfumo huo hautawahusu wale ambao tayari wana vitambulisho na wanahitaji kuvihuisha ifikapo Januari 2023 kwani watalazimika kwenda moja kwa moja ofisi za Nida kwa ajili ya kuingiza baadhi ya taarifa mpya na kupiga picha.


“Mfumo huu unalenga kupunguza usumbufu kwa waombaji wa vitambulisho vya taifa ambao kwa sasa wanalazimika kufika ofisi za Nida kuchukua fomu za maombi lakini kupitia mfumo huu mtu atajisajili popote kwa kutumia kifaa chenye uwezo wa kupokea mtandao wa mawasiliano,” amesema Tengeneza.

Amesema baada ya kujaza fomu, mwombaji atatakiwa kuchapa fomu na kuipeleka Serikali ya mtaa anapoishi kwa ajili ya kuthibitisha ukaazi wake kisha atatakiwa kupeleka fomu yake ofisi za Nida iliyopo wilaya anayoishi.

Meneja usajili na utambuzi Nida, Julien Mafuru amesema mfumo huo utapunguza muda unaotumika katika kusajili taarifa za mwombaji kwa kuwa usajili wa taarifa za mwombaji utakuwa umefanywa na mwombaji mwenyewe.


“Pamoja na kurahisisha huduma ya usajili kwa raia na wageni wakaazi, utapunguza pia gharama zinazotumika katika kuchapisha fomu za usajili na gharama za uchakataji wa taarifa,” amesema Julien.




Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad