Walioua bila kukusudia kwenye ‘kigodoro’ jela miaka 3
MKAZI wa Tegeta, Nassoro Hamadi (27), amehukumiwa kifungo cha miaka mitatu gerezani, baada ya kupatikana na hatia ya kumuua bila kukusudia Tamimu Athuman kwa kinachodaiwa ni wivu wa mapenzi.
Pia mahakama katika shitaka hilo imemhukumu Rajabu Juma (24), kifungo cha miaka miwili jela, Hassan Salum(25) na Hassan Hamad(23), wamehukumiwa miezi sita, ambao walishirikiana na mshitakiwa namba moja kutekeleza mauaji.
Washitakiwa hao wamesomewa hukumu hiyo leo na Hakimu Mkuu Mkazi, Richard Kabate, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
Akisoma hukumu hiyo , Kabati alisema kuwa maeneo ya Boko Chasimba, walimshambulia Tamimu Athuman kwa kumchoma kisu sehemu mbalimbali katika mwili wake.
“Oktoba 29, mwaka 2016 mshitakiwa namba moja Nassoro Hamadi majira ya saa moja usiku akiwa na wenzie kwenye ngoma ya kigodoro, alimtongoza Rehema Mohamed na wakakubaliana kuwa wote kwa usiku mzima, lakini ilipofika saa saba usiku walishangaa kumuona Rehema akiondoka na mwanaume mwingine ndipo walimfuata na kumuuliza kwa nini anaondoka na mwanaume huyo.
“Baada ya Rehema kumkataa Nassoro ndipo walipoanza kumshambulia Tamimu Athuman kwa kumchoma kisu na kuondoka eneo hilo, ” alisema Kabati.
Alidai kuwa marehemu alipelekwa hospitali ya lugalo, ambapo madaktari walithibitisha amefariki baada ya kutokwa na damu nyingi kwenye majeraha yaliyokuwa mwilini mwake.