WANASHERIA wa kujitegemea wamesema aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad, anapaswa kulipwa mishahara yake yote na malipo mengine kwa kipindi chote alichokuwa hayuko kazini hadi mwaka 2026 kwa sababu aliondolewa kinyume cha Katiba.
aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Assad.
Wanasheria hao kwa nyakati tofauti, waliyasema hayo jana ikiwa ni siku moja baada ya hukumu kutolewa na Mahakama Kuu Masijala Kuu, mbele ya majaji Dk. Benhaji Masoud, Juliana Masabo na Edwin Kakolaki.
Akizungumzia hilo, Wakili Frank Chacha alisema, Prof. Assad ana haki ya kudai mishahara yake yote, kiinua mgongo kama mtumishi mwingine ambaye aliondolewa kazini kinyume cha utaratibu.
Wakili Majura Magafu, akizungumzia uamuzi huo alisema Prof. Assad anaweza kuzipata haki zake kwanza, kwa kuangalia barua yake ya uteuzi ilivyoeleza kuhusu haki zake endapo ataachishwa kazi.
"Suala la kwanza la kuangalia ni ile barua yake ya uteuzi inaeleza nini. Je, atapata haki zipi endapo ataachishwa kazi na suala la pili, Prof. Assad ana haki ya kudai haki zake kwa sababu nafasi yake ni ya kikatiba na kuondolewa kwake Katiba ilitakiwa kufuatwa," alisema Magafu.
Wakili Edson Kilatu akichangia hoja alisema alipokea vizuri uamuzi wa Mahakama Kuu kwa sababu unaanza kuwakumbusha misingi ya Katiba ambayo inatakiwa kuzingatiwa na kutiiwa pasipokuwa na shaka.
"CAG ni nafasi nyeti haitofautiani na majaji wa Mahakama Kuu au Mahakama ya Rufani kwa sababu ya nafasi aliyo nayo ndiyo maana Katiba imemwekea kinga kwamba ukitaka kumtoa lazima kufuata taratibu ambazo Katiba inataka zifuatwe.
"Kifungu cha 6 (1) cha Sheria ya Ukaguzi kinaruhusu mkaguzi kupewa mkataba wa miaka kama mitano baada ya hapo inawezekana akaongezewa au asiongezewe wakati Katiba inataka akishika nafasi hiyo atumikie mpaka atakapofika umri wa kustaafu, ndiyo maana kwenye uamuzi wa mahakama imesema, kwanza imetengua hicho Kifungu.
"Lakini cha pili ikasema kwa sababu kwa mujibu wa Katiba ilitakiwa Assad aendelee kubaki kwenye nafasi yake mpaka anapofikisha umri wa kustaafu. Sasa aliondolewa kabla ndiyo maana mahakama imesema uamuzi wa kumtoa ulikuwa kinyume cha Katiba ya nchi.
"Suala ambalo limezua mjadala ni lile la kwamba baada ya kuwa mahakama imeona aliondolewa kimakosa pamoja na kwamba imekataa kusema na huyu aliyepo sasa kwamba yupo kinyume cha Katiba na imesema kwamba uteuzi wake ulifuata misingi inayotakiwa na vigezo vyote ambavyo alitakiwa awe navyo, alikuwa navyo. Kwa hiyo mahakama imeishia kusema Assad alitolewa kimakosa lakini imekataa kusema huyu aliyeingia aliingia kimakosa.
"Changamoto inakuja sasa unafuu upi ambao Profesa Assad anatakiwa aupate. Bahati mbaya wakati wa kesi inafunguliwa msingi uliokuwapo ni wa kutamka tu kwamba alitolewa kimakosa. Hawakwenda mbali kwamba kama mahakama itaona hapana sababu za kumrudisha kwenye nafasi yake labda alipwe fidia, mishahara yake aliyotumikia, sasa bahati mbaya kesi ya kikatiba haiendi huko.
"Mahakama haiwezi kutoa uamuzi zaidi ya kile ambacho hakipo mbele ya mahakama. Sasa hiyo hoja haikuwapo ndiyo maana mahakama iliishia pale,"alisema Kilatu.
Alisema changamoto iliyopo ni kwamba alitakiwa aunganishe na maombi ya fidia lakini pia kwa sababu ni shauri la kikatiba, maombi kwenye mashauri ya kikatiba yana mipaka yake kwa hiyo mara nyingi haiwezi kwenda kwenye kiwango cha fidia labda kama angefungua kesi ya aina nyingine.
Prof. Assad aliyeteuliwa mwaka 2014, aliondolewa katika nafasi yake Novemba, 2019 na alitakiwa kuendelea kuwepo kwa mujibu wa Katiba hadi 2026 atakapokuwa amefikisha umri wa kustaafu wa miaka 65.