Wasiojulikana Waiba Mtoto Mchanga



MTOTO Benitha Benedict, mwenye umri wa mwezi mmoja ambaye ni mtoto wa Joanitha Agustina, mkazi wa Mtaa wa Migera, Kata ya Nshambya, Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, ameibwa na watu wasiojulikana wakati mama huyo alipokuwa akiwasindikiza wageni.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo juzi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, William Mwampaghale, alisema tukio hilo lilitokea Desemba Mosi mwaka huu majira ya saa sita kamili mchana nyumbani kwa mama huyo.

Mwampaghele alisema kwa mujibu wa maelezo ya mama wa mtoto huyo kwa jeshi hilo, akiwa nyumbani anaendelea na shughuli zake, mwanawe alikuwa amelala chumbani wakati huo akipokea wageni watatu wanawake waliofika kwa lengo la kumpongeza kwa kujifungua.

"Akiwa anawasindikiza watatu hao, walikuja tena watu watatu kumtaka mazungumzo akawajibu kwamba hakuwa na mazungumzo nao na akaamua kuendelea na kuwasindikiza wageni wake, wakati anarudi nyumbani akitoka kusindikiza wageni wa awali aliingia ndani mpaka chumbani alipokuwa amelazwa mtoto, hakumwona tena," alisema.

Kamanda Mwampaghale alisema jeshi hilo linaendelea na uchunguzi wa kubaini waliohusika na wizi wa mtoto huyo na kuwataka wananchi kutoa taarifa kuhusu mtu yeyote wanayemtilia shaka.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad