Mwanza. Jeshi la Polisi mkoani Mwanza linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za mauaji ya Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT) Mwanza, Hamida Mussa (64).
Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Desemba 1, 2022, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amewataja miongoni mwa waliokamatwa kuwa ni pamoja na Sara Mwendeshasahani (15) aliyekuwa mfanyakazi wa ndani wa marehemu.
Mwili wa mhadhiri huyo ulikutwa Jumanne Novemba 29, 2022 nyumbani kwake Mtaa wa Buzuruga Mashariki wilayani Ilemela mkoani Mwanza ukiwa umelala sakafuni kifudifudi ukiwa na mtandio shingoni huku mfanyakazi wa ndani wa mhadhiri huyo akidaiwa kutokomea kusikojulikana.
Jana, akizungumza na Mwananchi, Mtoto wa mhadhiri huyo, Rehema Mbaga alisema taarifa ya mama yake kutoonekana aliipata Jumatatu kutoka kwa mmewe ambaye alikuwa na ahadi ya kukutana naye siku hiyo bila mafanikio.
"Mme wangu alivyompigia bila mafanikio aliniambia ikabidi nimpigie jirani yake, Tatu Issa ambaye naye alifika na kugonga mlango lakini haukufunguliwa, kwa sababu ilikuwa jioni tulidhani labda ametingwa na majukumu yake ya ufundishaji tukasema tumtafute kesho yake (juzi Jumanne)," alieleza
Alisema akiwa na mmewe, juzi Jumanne waliamkia nyumbani kwa Hamida na kukuta mlango umefungwa ndipo wakaomba kibali cha kuvunja mlango wakiwa na askari wa Polisi wa kituo cha Buzuruga na kukuta mwili wa mama yake ukiwa sakafuni.
"Tulipopekua tulikuta miguu ikiwa koridoni huku sehemu nyingine ya mwili ikiwa chumbani kama alikuwa anajibuta hivi lakini mfanyakazi wa ndani hatukumpata na kadi za benki za marehemu nazo hazionekani zilipo," alisema
"Baada ya hapo Polisi walichukua mwili na kuupeleka Bugando kwa uchunguzi zaidi ambao umeonyesha alifariki kwa kunyongwa shingoni," alisema Rehema