Dar es Salaam. Tukiwa katikati ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, Mkuu wa Wilaya Songwe, Simon Simalenga ametuhumiwa kumshambulia kwa ngumi na kumjeruhi msichana, Frolensia Mjenda (20) kwa kosa la kukaa juu ya jukwaa.
Kufuatia sakata hilo leo Jumanne, Desemba 6, 2022 Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Doroth Gwajima amesema aliunda kikosi cha maofisa ustawi wa jamii mkoa wa Songwe ambacho tayari kimeleta mrejesho.
“Tukio ni la kweli, binti ana miaka 20 na ameshafungua kesi ya shambulio la aibu namba Mkw/IR/1149/2022 polisi kituo cha Mkwajuni. Nimetuma tena kikosi hicho kiende kijijini nyumbani kwa binti huyu wampe ushauri nasihi wakati shauri likiendelea. Aidha wasaidizi wa kisheria wafuatilie kwa karibu hatua zote,” amesema Gwajima na kuongeza;
“Binafsi nimesikitishwa na tukio hili, nakemea viongozi kwenda nje ya utaratibu na kuanza ugomvi binafsi na wananchi ambapo wanawake, wasichana na watoto wanakua wahanga zaidi. Haikubaliki.”
Juhudi za kumtafuta Simalenga hazikuzaa matunda baada ya simu yake kuita bila kupokelewa na baadaye ilikuwa ikikatwa.
Binti huyo Frolensia Mjenda anayeishi Kata ya Mbangala wilayani Songwe amesema walienda eneo hilo kwa ajili ya mchezo wa mpira na baada ya mechi kumalizika walipumzika jukwaani kabla ya kiongozi huyo kutokea.
“Wakati tumepumzika, Mkuu wa Wilaya alituita wenzangu walinizunguka nikaenda kumsikiliza nikampa heshima yake kama ni mtu mkubwa nilipofika pale akanishika mkono na kuanza kunipiga nikamuomba msamaha kwamba mimi ni mgeni.
“Wakati ananipiga hakusema chochote baadaye akatuita wote na kuanza kutuelekeza kwamba hili jukwaa hatukutengeneza kwa ajili ya kukaa watu alipomaliza akasema hili jukwaa nalifungia. Nikaenda nyumbani wazazi hawapo nikalala asubuhi wazazi wamerudi nikawalekeza kilichonitokea,” alisema Flolensia
Endelea kusoma mitandao yetu kwa taarifa zaidi