Wakati Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likitupiana mpira na Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji juu ya trehe halisi ya marudio ya hukumu ya kesi ya kiungo Feisal Salum 'Fei Toto' na klabu ya Yanga, Mwanaspoti linajua kwa mujibu wa kanuni akishinda kesi hiyo atakuwa mchezaji huru, lakini hatacheza tena msimu huu kwenye klabu yoyote nchini.
Kwa mujibu wa kanuni za Ligi Kuu, haziruhusu mchezaji huru kujiunga na timu yoyote wakati msimu unaendelea, jambo litakalomfanya Fei kukaa nje ya uwanja hadi msimu ujao ajua pa kwenda hii ikiwa ni baada ya kuyagomea maamuzi ya Kamati ya Sheria ilimtambua bado ni mchezaji halali wa Yanga.
Fei alitibua na klabu hiyo aliyoichezea tangu mwaka 2018 kwa kutumia vipengele vya mkataba wake kuvunja kwa kuilipa Sh 112 Milioni zikiwa ni za kuvunjia mkataba na mishahara wa miezi mitatu, lakini mabosi wake wakamchomolea na kukimbilia TFF kushtaki.
Kamati hiyo ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji ilikutana mapema mwezi huu na kutoa maamuzi ya kumtambua Fei Toto kama mchezaji wa Yanga, licha ya kutotoa tena tamko lolote kama TFF ilivyoahidi, japo inaelezwa kiungo huyo alikataa kwenye utetezi wake na kusisitiza anasonga mbele.
Katika kuhakikisha anaitafuta haki yake mbele ya safari, Fei kupitia wanasheria wanaomsimamia waliomba marejeo ya hukumu hiyo ambayo walitumiwa kimya kimya, ili wajue pa kuanzia kama ni kwa kukata rufaa hapa hapa nchini ama waende Mahakama wa Usuluhishi ya Kimataifa ya Michezo (CAS), lakini hadi sasa hawajajibiwa na shirikisho hilo lililowatupia mpira kamati hiyo ya sheria.
Akizungumza mmoja ya mawakili wa upande wa kiungo huyo,Makubi Kanju Makubi alisema tayari walituma barua kwa TFF wakiomba marejeo ya hukumu hiyo, lakini hadi sasa hawajaambiwa itafanyika lini lakini wanaamini ni siku za hivi karibuni.
"Tuliwaandikia barua utawala tukiomba review, kwa maana utawala ndio unapeleka barua hiyo kwa kamati na kamati inapanga lini jambo hilo lifanyike lakini hadi sasa bado hatujajibiwa," alisema Makuki na kuongeza;
"Ujue mambo haya yanafuata utaratibu naamini wanalifanyia kazi ndani ya muda na siku si nyingi huenda wakatujibu tuakaendelea na taratibu nyingine, na tukiona wanachelewa basi tutawakumbusha."
Makubi alisisitiza Fei Toto anaendelea kusubiri, huku akifanya mazoezi binafsi kwani hajakubaliana na majibu ya kamati yanayomtaka kurudi Yanga na amesimamia msimamo wake hadi sasa wa kutorudi kwa Wanajangwani hao.
"Mchezaji (Fei Toto), anasubiri mustakabali wa shauri hilo, kwani hakuridhika na maamuzi ya awali, hivi sasa anaendelea na mambo yake mengine ikiwemo kufanya mazoezi binafsi na baada ya marejeo ya hukumu atajua nini kinaendelea na tutawajuza," alisema Makubi.
Kwa upande wa TFF kupitia kwa Mkurugenzi wa Sheria Habari na Masoko, Boniface Wambura alikiri kupokea kwa barua kutoka upande wa Fei na sasa taratibu nyingine zinaendelea.
"Ni kweli tulipata barua yao na sasa tunaendelea na taratibu nyingine. Kuna mambo mengi yanatakiwa kuwa sawa ili review ifanyike ikiwemo kupatikana kwa wajumbe wote wa kamati kwani sio kwamba wote wanakaa Dar es Salaam, hapana na wengi wao wanamajukumu mengine," alisema Wambura na kuongeza;
"Siwezi kukuahidi ni lini review hiyo itafanyika kwani hadi sasa badi sijawa na taarifa kamili lakini unachotakiwa kujua ni kwamba barua ya upande wa Fei tumeipata na taratibu nyingine zinaendelea."
Hata hivyo, hata kama Fei atafanikiwa kukubaliwa ombi lake la marejeo ya hukumu na akashinda kesi hiyo, bado hataweza kucheza tena msimu huu, kwani alishavunja mkataba kama walivyosimamia, huku dirisha la usajili likiwa limefungwa na kanuni zikiwa haziruhusu mchezaji huru kuingia katikati.
Kwa sasa kiungo huyo wa zamani wa JKU ya Zanzibar yupo visiwani humo akiendelea kujifua kwa mazoezi baada ya awali kwenda kujifua Dubai na kulazimika kurejea kuja kusikilizia kesi hiyo na Yanga.
Fei Toto ndo Hivyo Tena Hasikii la Mkubwa Wala la Mtoto, Yanga Waandike Maumivu