Aliyechonga kifimbo cha Nyerere afariki



Moshi. Kada maarufu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Omary Mwariko aliyewahi kujitokeza kuwania urais mwaka 2005 na ambaye ndiye aliyechonga kifimbo cha Baba wa Taifa la Tanzania, Mwalim Jullius Kambarage Nyerere, amefariki dunia.

Jina la Mwariko ni maarufu si tu kwamba alijitokeza ndani ya CCM kuwania urais mwaka 2005, lakini hotuba zake zilikuwa zikiwavutia wana CCM wengi na hata kusambaa katika mitandao ya kijamii kutokana na vichekesho vyake.

Katika kuomba kura kwa wana CCM katika kura za maoni kugombea ubunge Jimbo la Moshi mjini uchaguzi mkuu 2010 na 2015, moja ya ahadi yake ni kuwepa pazia kuuzunguka mlima Kilimanjaro, ili kuwazuia wakenya kutangaza ni wa kwao.

Mbali na hilo, lakini ni mgombea huyo ambaye alijinadi kuanzisha kiwanda cha kutengeneza vifaa vya kijadi vya kwenda anga za juu na pia kuanzisha hospitali maalum ambayo wachawi wote wataletwa pamoja ili kuagua wahitaji.


Pia akaahidi kama angechaguliwa kuwa Mbunge, angeifanyia mageuzi makubwa serikali ili binadamu wote wa Jimbo la Moshi mjini waweze kupokea mishahara kila Jumamosi na kwamba vijana wote wa Jimbo hilo wangepokea mishahara.

Hata hivyo, licha ya kuwa mmoja wa wagombea ambaye makada wa CCM walipenda kumsikiliza, lakini hata video fupi fupi (video clip) zilizokuwa zikimuonyesha akijinadi, zilikuwa zikisambaa kwa kasi katika mitanfao ya kijamii.

Taarifa za kifo chake

Taarifa za kifo cha mwanasiasa huyo, msanii na mwana utamaduni, zilianza kusikika leo Jumapili, Januari 22, 2023 kupitia mitandao ya kijamii na baadae mmoja wa watoto wake, Kennedy Mariko alilithibitishia gazeti hili kwa njia ya simu juu ya msiba huo.


“Ni kweli mzee amefariki na hapa tuko kwenye msiba hapa Mailisita (wilaya ya Hai). Mzee alikuwa na tatizo la moyo na iligundulika moyo wake ni mkubwa kwa hiyo jana (juzi) usiku ndio amefariki dunia hospitali ya KCMC,”alisema.

Kwa upande wake, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Moshi mjini, Athman Ally amesema taarifa za msiba huo alizipokea kutoka kwa familia na kwamba marehemu alikuwa ni kada mtiifu aliyeshiriki kikamilifu kukijenga chama cha Mapinduzi.

“Ninafahamu alikuwa na tatizo la moyo muda mrefu kidogo na alikuwa akihudhuria kliniki ya moyo kwenye hospitali ya Rufaa ya KCMC. Kiukweli tumeumizwa na msiba huu lakini yote ni mapenzi ya Mungu,” alisema Ally.

Alivyochonga kifimbo cha Nyerere

Katika mahojiano maalum aliyoyafanya na gazeti la Mwananchi 2008 wakati huo akiwa na umri wa miaka 59, alisema yeye ndiye alikuwa mchongaji wa kifimbo cha Nyerere, na kusema kifimbo hicho kilikuwa na nguvu ambayo si ya kichawi.


"Ni kweli ni kifimbo ambacho kilikuwa na nguvu ya pekee lakini hakikuwa na uchawi bali kilikuwa na nguvu za utamaduni wa Kiafrika…Nyerere alikuwa mtawala kwa hiyo alistahili kitu kilichomtambulisha kama mtawala,"alisema.

Katika mahojiano hayo, Mwariko alisema wazo la kumtengenezea Mwalimu Kifimbo cha aina hiyo alilipata mwaka 1972 mara baada ya kupata tuzo ya Jumuiya ya Madola kuwa msanii nyota wa bara la Afrika.

 "Nilipata tuzo hii kutoka kwa Malkia Elizabeth wa Uingereza baada ya kazi zangu kushinda katika maonyesho hayo ya kisanii yaliyofanyika Uingereza na kujulikana kama Commonwealth Art Gallery 1972,"alieleza mwana utamaduni hiyo.

Kwa mujibu wa Mwariko, aliporejea nyumbani ndipo alipoona heshima aliyopewa Uingereza isiishie hivi hivi ndipo alipobuni na kutengeneza kifimbo hicho ambacho alikipa jina la Kumekucha Afrika na ndio ukawa mwanzo wa kifimbo cha Nyerere.


Mwariko alibainisha kuwa mti uliotengenezea kifimbo hicho ni mti maalumu ambao anasema ni siri yake lakini akasema si mti wa kawaida kama hii inayotumika sasa kutengeneza vifimbo vya viongozi wengine wakiwamo polisi.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad