Aliyelazimisha Dawa Zilizoisha Muda Zitumike Matatani, Arekodiwa na Mwenzake

 


Serikali imesema itatoa taarifa juu ya hatua zilizochukuliwa kuhusu video inayosambaa mtandaoni ikimuonyesha muhudumu wa Afya mkoani Tabora akiwa kwenye majibizano na mwenzake, huku akilazimisha matumizi ya dawa zilizoisha muda wake.

Dar es Salaam. Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema Serikali inalifuatilia tukio la mhudumu wa afya mkoani Tabora aliyekuwa akilazimisha dawa zilizoisha muda wake zitumike kwa wajawazito lililoonekana kupitia video iliyosambaa mtandaoni.

Leo Januari 6, 2023 kupitia mtandao wa Twitter ilisambaa video ikimuonyesha mwanamke ambaye inasadikika ni mtaalamu wa afya, akijibizana na mwanaume ambaye hakuonekana kwenye video hiyo juu ya matumizi ya dawa zilizoisha muda wake.

Kulingana na maelezo yaliyoambatana kwenye video hiyo yenye urefu wa dakika 48, mwanaume anayesikika kupinga matumizi ya dawa hizo ni mtaalamu wa maabara huku anayelazimisha zitumike ni muhudumu wa afya.

Katika majibizano hayo ambayo muhudumu huyo wa afya akiwa ameketi (mwanamke) anaonekana akimtolea maneno makali mtaalamu huyo wa maabara (mwanaume) akimwambia ana kiherehere cha kutotaka dawa hizo zitumike.

Kupitia video hiyo iliyorekodiwa kwa usiri, majibizano yao yalikuwa kama ifuatavyo:

Mhdumu wa afya: Unampima mtu afya?

Mtaalamu wa maabara: Dawa hizi zimekwisha wakati wake.

Muhudumu wa afya: Mbona una kiherehere sana unataka ufanyakazi bora?

Mtaalamu wa maabara: Zilezile sizitumii zimeisha wakati wake.

Mhudumu wa afya: Tumeambiwa watumie wajawazito.

Mtaalamu wa maabara: Situmiii situmii.

Mhudumu wa afya: Nenda kamwambie ‘in-charge’ usiniambie mimi.

Mtaalamu wa maabara: Nishakuambia wewe kwa sababu ndio unalazimisha muhudumu wa afya, aaah mwanaume gani wewe unakuwa na shobo? Wewe ndio mtaalamu tangu taasisi imeanza nyo-nyo-nyo acha usipime wewe ndio unajua miongozo sana pita hivi!

Mtaalamu wa maabara: Kila mtu atumie taaluma yake vizuri mhudumu wa afya una utaalamu.

Kufuatia video hiyo Waziri Ummy kupitia ukurasa wake wa Twitter amesema Serikali inafuatilia suala hilo.

“Timu ya Usimamizi Afya ya Mkoa (RHMT) wa Tabora na ya Halmashauri (CHMT) ya wilaya ya Uyui wanafuatia suala hili. Serikali itatoa Taarifa kwa umma juu ya hatua zilizochukuliwa,” ameandika.

Ameendelea kusema kuwa Tanzania ina vitendanishi vya kutosha vya kupima malaria (MRDT) ambavyo havijaisha muda wake vya kutosheleza miezi sita.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad