Askari Tanapa auawa kwa kuchomwa mshale wenye sumu



Musoma. Afisa uhifadhi wa wanyamapori daraja la kwanza wa hifadhi ya Taifa ya Serengeri, Deus Mwakajegele ameuawa kwa kuchomwa mshale na watu wasiojulikana alipokuwa akitekeleza majukumu yake.

Tukio hilo limetokea jana Jumamosi Januari 21, 2023 katika eneo la Nyanungu wilayani Tarime baada ya kuchomwa mshale wenye sumu kichwani na kufariki katika hospitali ya Seliani Arusha alipopelekwa kwa ajili ya matibabu.

Akizungumza kwenye ufunguzi wa wiki ya sheria mjini Musoma leo Jumapili Januari 22, 2023, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mzee amesema kuwa tukio hilo limetokea katika eneo lililokuwa na mgogoro ambao ulikuwa umetolewa maamuzi na vyombo vya dola.

"Nimesikitika sana yaani wananchi wamefikia hatua ya kumchoma askari mshale wenye sumu akiwa anatekeleza majukumu yake, hii ni mbaya sana" amesema.


Amesema mtu mmoja amekamatwa na jeshi polisi huku uchunguzi wa kina ukiendelea kufanyika kuwabaini wahusika.

Akifafanua mgogoro uliopo katika eneo hilo, amesema kwa muda mrefu wananchi wa Kata ya Nyanungu na maeneo jirani wamekuwa wakiingiza mifugo ndani ya eneo hilo ambalo lipo ndani ya hifadhi ya Serengeti jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

"Pamoja na kamati ile ya mawaziri wanane kupita hakuna mabadiliko yaliyotokea maana yake ni kwamba eneo hilo bado lipo ndani ya hifadhi sasa wananchi wanashinikiza waruhusiwe kuingia ndani kuchunga mifugo yao kwa sababu pale kuna malisho mazuri na lile eneo ni eneo muhimu kwa mzunguko ule wa uhamaji wa nyumbu" amesema.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad