Shirika la Utangazaji la Uingereza(BBC) limeomba radhi baada ya kelele za ngono kusikika wakati wa matangazo ya michuano Kombe la FA. Sauti hizo zilisikika wakati mchanganuzi wa soka Gary Lineker alikuwa akichambua mechi ya marudiano ya raundi ya tatu kati ya Wolves na Liverpool siku ya Jumanne, Januari 17.
Lineker hata hivyo, alijaribu kupuuza kelele hizo wakati wa kipindi hicho kilichopeperushwa mubashara kwenye Uwanja wa Molineux. “Tunaomba radhi kwa watazamaji wote walioudhika wakati wa matangazo ya moja kwa moja ya kandanda jioni hii.” BBC ilisema katika taarifa kupitia kwa msemaji wake ikiongeza kuwa tukio hilo linachunguzwa. Baadaye Lineker alichapisha picha ya simu ya rununu kwenye mtandao wa kijamii akisema ilirekodiwa nyuma ya seti.