CUF yatangaza kufanya mikutano ya hadhara, Prof. Lipumba kuunguruma Manzese kesho




CHAMA cha Wananchi (CUF), kimetangaza kuanza mikutano ya hadhara huku kikiagiza matawi yake kuandaa mikutano hiyo. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza na wanahabari leo Ijumaa, tarehe 6 Januari 2022, Naibu Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF, Yusuph Mbungiro, amesema mkutano huo utaanza kesho Jumamosi, katika Wilaya ya Ubungo, ambao utafanyika katika Uwanja wa Bakhresa, Manzese jijini humo.

“Tutumie nafasi hii ya kuondokewa zuio la mikutano, ni vyema wanachama kujenga hamasa kuhakikisha mikutano ya hadhara inaandaliwa,” amesema Mbungiro.

Mbungiro amesema “Tutafanya mikutano ya hadhara kwa ustaarabu, hatutakashifu watu mikutano yetu itakuwa ya kunadi sera za chama chetu, kukosoa Serikali inapokosea, kusimamia ujenzi wa demokrasia katika taifa letu.”


Katika hatua nyingine, Mbungiro amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuondoa zuio la mikutano ya hadhara lililowekwa na mtangulizi wake, Hayati John Magufuli, akisema litasaidia kutibu majeraha ya wananchi waliyonayo kwa takribani miaka sita, kwa kukosa nafasi ya kusikia sera za vyama vya upinzani.


“Tunampongeza Rais Samia Kwa kutembea kwenye maneno yake na kuwa msikivu sababu mara kadhaa CUF ilimshauri aheshimu Katiba na Sheria za nchi lakini ajenge utawala Bora,” amesema Mbungiro.

Amesema mikutano ya hadhara itasaidia kuimarisha misingi ya demokrasia na utawala bora, pamoja na kusaidia vyama vya siasa kutangaza sera zake kwa wananchi.

Aidha, Mbungiro amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama visiwe sababu ya kuzuia mikutano hayo kinyume cha Sheria kwa kuwa kazi yao ni kulinda mikutano hiyo.

Naye Katibu wa CUF Wilaya ya Ubungo, Masoud Matemanga, amesema mgeni rasmi katika mkutano huo ni Mwenyekiti wa CUF Taifa, Prof. Ibrahim Lipumba.

Matemanga amesema mkutano huo utaanza asubuhi lakini viongozi wa CUF wataanza kuzungumza kuanzia saa 8.00 mchana hadi 12.00 jioni.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad