Mwaka huu 2023 kiburudani ulifunguliwa kwa ;’uchokozi’ wa Uongozi wa Wasafi Classic Baby (WCB) kumtibua na kumkasirisha Msanii Alikiba.
Msanii Alikiba alionyesha kuchukizwa na kile walichofanya meneja wa Diamond Platnumz na WCB Wasafi, Sallam SK kwa kutoa kile alichoita orodha ya wasanii waliofanya vizuri mwaka 2022 hivyo kuibua bifu jipyaa.
Katika orodha mbili za Sallam SK alimtaja Diamond kama msanii namba moja huku Alikiba akishika nafasi ya saba, hili ndilo lilimtibua Ali Kiba na akasema huo ni mwendelezo wa kiki kwa Wasafi.
Ikumbukwe Diamond na Alikiba wamekuwa wakitajwa kama washindani wakubwa kwenye muziki wa Bongo Fleva, wanatajwa kuvuna mashabiki wengi waliounda kambi mbili, hivyo kuchochea ushindani wa wasanii hao.
Ni wasanii ambao wametofautiana kwa mambo mengi katika muziki wao na mambo mengine yanayoshabiana na kazi yao iliyowapatia umaarufu.
Diamond Platnumz.
Tukichambua tabia za wasanii hawa ni kwamba tangu anaanza muziki Alikiba hajawahi kufungiwa wimbo wake wowote na Baraza la Sanaa Taifa (Basata) na akasema hutengeneza muziki ambao hata mama yake mzazi anaweza kuusikiliza na video ambazo hata watoto wanaweza kuzitazama wakiwa na wazazi wao.
Kwa upande wa Diamond, nyimbo zake mbili, ‘Hallelujah’ na ‘Waka’ zimefungiwa na Basata kutokana na kukiuka maadili ya Tanzania, huku wimbo ‘Mwanza’ alioshirikishwa na Rayvanny ukifungiwa pia, na hata video ya wimbo wake ‘Mtasubiri’ aliomshirikisha Zuchu nayo imefungiwa kwa kukosa maadili!.
Kuhusu albamu, Diamond ametoa albamu tatu; Kamwambie (mwaka 2010), Lala Salama (2012) na A Boy From Tandale (2018), huku akitoa na EP moja, First of All (2022).
Kwa upande wa Alikiba naye ana albamu tatu sawa na Mondi ambazo ni; Cinderella (mwaka 2007), Ali K 4Real (2009) na Only One King (2021), tofauti ni kwamba Kiba hana EP ingawa ndiye wa kwanza kutoka kimuziki kabla ya Diamond. Amemzidi Mondi kwa zaidi ya miaka mitano.
Kwa upande wa tuzo ni zaidi ya miaka nane bado Diamond anashikilia rekodi ya kushinda tuzo saba za Muziki Tanzania (TMA) 2014 kwa usiku mmoja, Alikiba amejaribu kuvuja rekodi hii mara mbili bila mafanikio.
Mwaka 2015 Alikiba alikaribia kuivunja rekodi hiyo ya Diamond lakini akaishia kushinda tuzo tano tu kwa usiku mmoja, na mwaka jana ziliporeja tena tuzo hizo baada ya miaka saba, Alikiba alishinda tano, hivyo hajavunja rekodi ya Diamond kwa upande wa tuzo hizo.
Kuhusu kufanya kazi na akina mama, Alikiba amewahi kufanya kazi na wanawake wawili ambao wamewahi kuwa na mahusiano na Diamond hadi kujaliwa watoto, wanawake hao ni Tanasha Donna kutokea Kenya aliyejaliwa mtoto mmoja, Nasseb Junior, katika video ya wimbo wake, ‘Nagharamia’, pia alimtumia Hamisa Mobetto mwenye mtoto mmoja na Diamond, Dylan, katika video ya wimbo wake, ‘Dodo’, lakini Diamond hajafanya kitu kama hicho.
Lebo ya Diamond, WCB inasimamia wasanii watano wakiwemo wawili wa kike, wakati Kings Music ya Alikiba ina wasanii wanne na hakuna hata mmoja wa kike.
Wasanii hawa wamedhihirisha kuwa damu ni nzito kuliko maji kwani wote wamewasaini ndugu zao kwenye lebo zao za muziki, Diamond kamsaini dada yake, Queen Darleen, huku Alikiba akifanya hivyo kwa mdogo wake, Abdukiba.
Baada ya mwaka jana Alikiba kushinda tuzo tano za TMA alifikisha jumla ya tuzo 17 za TMA sawa na Diamond mwenye 17 pia.
Takribani miaka 20 katika Bongo Fleva, Alikiba hajawahi kurekodi wimbo au video na mwanamke yeyoye aliyewahi kuwa naye katika mahusiano au ndoa.
Ila Diamond kafanya hivyo na Tanasha Donna kupitia wimbo wao ‘Gere’ na Hamisa Mobetto kupitia wimbo ‘Jibebe’, pia Hamisa ndiye katokea kwenye video ya wimbo wake, ‘Salome’, huku Zari The Bosslady kwenye video za nyimbo, ‘Utanipenda’ na ‘Iyena’.
Bila shaka umeona tofauti kubwa ya wasanii hawa wanaotingisha kwenye muziki wa Bongo Fleva Tanzania.
Na Elvan Stambuli