Ishu ya kiungo mshambuliaji Feisal Salum 'Fei Toto' ya kuvunja mkataba na Yanga, imewashitua wadau wa soka nchini, huku ikizua mjadala kuutafsiri mkataba wake namna ulivyotoa funzo kwa wachezaji wenzake wazawa.
Si rahisi sana kwa mchezaji mzawa kufanya maamuzi kama ya Fei Toto tena akiwa Yanga, ilihitaji ujasiri unaosukumwa na kufikiria hatma ya maisha yake ya baadaye, baada ya umaarufu mkubwa anaoupata kupitia kipaji chake, akitundika daruga je bata zake zitakuwa za kulia kivulini? ama bado ataendelea kusaka juani.
Halina kificho kwamba mchango wa Fei Toto pale Yanga ulikuwa muhimu na alikuwa kipenzi cha mashabiki, hivyo isingekuwa kuwaza maisha na fursa anazozipata asingethubutu kuwaudhi wafuasi wa timu hiyo.
Licha ya timu mojawapo ya Ligi Kuu (jina tunalo) inayotajwa kumsajili Fei Toto kutosema lolote, ukweli ni kwamba imeipiga Yanga na kitu kizito cha kumalizia nacho mwaka 2022 na kuingia 2023 na kumbukumbu ya maumivu.
Fei mwishoni mwa mwaka jana wakati sakata lake linaendela alienda nje ya nchi kwa ajili ya mapumziko mafupi huku ikisemekana timu inayotajwa kumsajili ilimtafutia kocha wa kumfundisha pia itasaka klabu atakayokuwa anafanya nayo mazoezi ya kulinda kiwango chake.
Hata hivyo haikuchukuwa muda mrefu kurejea nchini baada ya Kamati ya Sheriana Hadhi za wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kumtumia wito wa kuhitajika baada ya mabosi wake Yanga kupeleka malalamiko yao juu ya mchezaji huyo kuhusu kuvunja mkataba wake na klabu hiyo wakidai haujafuata taratibu.
Juzi, Kamati hiyo ilitarajiwa kutoa maamuzi yao baada ya kikoa chao kilichofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita kwa kuwakutanisha Yanga na Fei Toto.
Baada ya kutokea ishu ya Fei Toto, Makala hii imekukusanyia baadhi ya sajili nyingine ambazo zimewahi kuumiza mioyo ya mashabiki wao kwa nyakati tofauti, kutokana na wachezaji waliowapenda kuhamia timu nyingine.
AMISSI TAMBWE
Usajili wa straika Amissi Tambwe kutoka Simba msimu wa 2014-2019 kwenda Yanga uliwaumiza mashabiki na kushindwa kuelewa nini kimetokea staa huyo kuondoka kirahisi akiwa ameibuka kinara wa mabao 19 (2013/14).
Mashabiki hao walizidi kuumia zaidi baada ya Tambwe kufanya vizuri Yanga, jambo ambalo liliwapa sintofahamu ya kwa nini viongozi walishindwa kumbakiza mshambuliaji aliyekuwa tegemeo ndani ya timu.
BERNARD MORRISON
Habari za winga Bernard Morrison kutua Simba msimu wa 2020-2022 ziliitikisa Yanga hadi kufikia hatua ya kupeleka mashitaka TFF na baada ya kushindwa ikakata rufaa chombo kingine cha juu CAS ambako nako ikagonga mwamba na kufanya mashabiki kuumia zaidi.
Kilichokuwa kinawaumiza mashabiki wa Yanga ni ufundi, kiwango cha juu zikiwemo mbwembwe alizokuwa anazionyesha Morrison, hivyo kila alipokuwa akicheza alikuwa anazomewa. Hata hivyo kibao kimewageukia wafuasi wa Simba baada ya staa huyo kurejea tena Jangwani nao walijikuta wakiangukia maumivu.
GADIEL MICHAEL
Usajili wa beki Gadiel Michael kutoka Yanga 2017 na kutua Simba anayoitumikia hadi sasa uliwakera mashabiki wa Yanga, kwani kipindi hicho alikuwa kwenye kiwango kikubwa na hakuwa anakosekana kwenye kikosi cha Stars, hivyo bado walitamani kuendelea kupata huduma yake.
Ingawa kwa sasa mashabiki wa Yanga wana raha kuona Gadiel anakosa nafasi mbele ya Mohamed Hussein 'Tshabalala' ambaye kila kocha anayekuja anamwamini kikosi cha kwanza.
HARUNA NIYONZIMA
Kitendo cha kiungo fundi, Haruna Niyonzima kutua Simba 2017-2019 akitokea Yanga kiliwapa maumivu makali mashabiki wa Wanajangwani ambao baadhi yao kwa hasira walichoma jezi zilizokuwa zimeandikwa jina lake.
Ni usajili ulichukua muda mrefu kujadiliwa hadi pale alipoonekana na jezi ya Simba kwenye mazoezi, lakini bado wafuasi wa Yanga waliendelea kunung'unika, wakimuombea asifanikiwe ni kweli hakucheza kwa kiwango kilichozoeleka.
KELVIN YONDANI
Kama kuna taarifa zilikuwa ngumu kukubaliana nazo mashabiki wa Simba 2012 ni za aliyekuwa beki wao wa kati, Kelvin Yondani kutua Yanga ambako alitumika miaka tisa tangu alipojiunga nao 2012-2020 baadaye akaachana na Wanajangwani na kujiunga na Polisi Tanzania na kwa sasa yupo Geita Gold.
JUMA KASEJA
Wakati kipa Juma Kaseja akiwa kwenye kiwango cha juu, Yanga ilimnyakua kutoka Simba msimu wa 2014/15 jambo ambalo liliwapa maumivu makali mashabiki ambao walikuwa wanamuita Tanzania One, kutokana na kuwa panga pangua kwenye kikosi chake na Stars.
FRANK DOMAYO
Wakati Azam FC inamsajili Domayo 2014-2021 alikuwa kwenye kiwango cha juu na bado huduma yake ilikuwa ikihitajika na Yanga, hilo liliwafanya mashabiki kuumizwa na kuondka kwake.
MBUYU TWITE
Kama kuna mwaka Simba ilikosa amani ni 2012 siku moja kabla ya Yanga kumsainisha beki Mbuyu Twite akitokea APR ya Rwanda, aliyekuwa Mwenyekiti wa Simba Aden Ismail Rage alipiga picha na mchezaji huyo akiwa na jezi ya Simba.
Simba nayo ilikuwa inafukuzia saini ya Twite lakini Yanga ikawapiga bao kwa kumchukua beki huyo na aliichezea klabu hiyo kwa kiwango cha juu, jambo lililokuwa linawapa wakati mgumu mashabiki na viongozi kutaniwa na watani wao wa jadi, ingawa hadi sasa kuna wakati kumbukumbu hiyo inafufuliwa na kutolewa mfano.
ATHUMAN IDD 'CHUJI'
Ni kiungo ambaye alikuwa bado anahitajika ndani ya Simba lakini mwaka 2006 aliamua kuachana na timu hiyo ambapo alitimkia Yanga kwa watani zao, mashabiki walikuwa wanahitaji huduma ya kiungo huyo bora nchini kwa wakati huo lakini hakukuwa na namna yoyote ya kumbakiza kwao.
Chuji aliamua kuondoka ndani ya Simba ikidaiwa kutokuwepo kwa maelewano mazuri na baadhi ya mabosi wake, kitu ambacho aliona hakitakuwa na afya kuendelea kuwepo kikosini humo.
Usajili mwingine ulikuwa ni wa Ibrahim Ajibu kutoka Simba kwenda Yanga, Didier Kavumbagu kutoka Yanga kwenda Azam FC, Moses Phiri kutarajiwa kutoa Yanga akajiunga na Simba,Aziz Ki kutua Yanga badala ya Simba hao ni baadhi tu kati ya wale ambao waliwaumiza mashabiki wao.