John Mnyika "Katiba ni Kipaumbele"




Dar/Mwanza. Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika amesema ajenda yao katika mikutano ya hadhara watakayoifanya katika maeneo mbalimbali nchini ni kudai Katiba mpya na Tume huru ya uchaguzi hadi kieleweke.

Mnyika, ambaye ni mbunge wa zamani wa majimbo ya Kibamba na Ubungo, mkoani Dar es Salaam alisema pamoja na mambo mengine yanayohusu wananchi, lakini suala la Katiba mpya na Tume huru ya uchaguzi ndizo ajenda zao kuu.

“Tunaelekea mwaka 2024 na 2025 ambayo ipo karibu, ajenda yetu kuu Chadema katika kila mikutano yetu ya hadhara ukiondoa masuala mengine ya wananchi, itakuwa Katiba mpya na Tume huru ya uchaguzi,” alisema Mnyika.

Mnyika alitoa kauli hiyo juzi, katika ufunguzi wa mikutano ya hadhara kwa chama hicho, uliofanyika uwanja wa Furahisha Jijini Mwanza ambapo pia walikuwa wakisherehekea Chadema kutimiza miaka 30 tangu kilipopata usajili wa kudumu Januari 21, 1993.


“Sasa ni bahati mbaya muda umesogea leo ni Januari 21, sasa tunataka kuona utayari wa Serikali wa kupeleka bungeni muswada wa kuuendeleza mchakato wa Katiba mpya, kama ambavyo Rais Samia Suluhu Hassan alivyoonesha utayari wa kuendeleza suala hili,” alisema Mnyika.

Mnyika alisema, “Mwenyekiti tunakuomba utangaze kuanzia leo na kila Januari 21 kuwa ni ‘Siku ya Chadema’ ili kila mtu atakapokuwa katika siku hii ataikumbuka siku iliyoanzishwa Chadema”.

Kauli ya Mnyika kuhusu mchakato wa kudai Katiba mpya inapata nguvu zaidi baada ya Rais Samia, akiwa na viongozi wa vyama vya siasa 19 vyenye usajili ya kudumu, Ikulu jijini Dar es Salaam Januari 3, mwaka huu kuahidi kuukwamua mchakato wa marekebisho ya Katiba kwa namna watakavyokubaliana kwa siku za usoni.


Hoja ya Mnyika

Katika hotuba yake jana, Mnyika alisema wangependa kuona Serikali ikipeleka muswada bungeni wa kuendeleza na kukamilisha mchakato wa Katiba mpya, kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025. Mnyika alisema kipaumbele cha Taifa kwa sasa ni Katiba mpya na Tume huru ya uchaguzi.

Hata hivyo, Mnyika alisema pamoja na kwamba wanaendelea kudai Katiba mpya na Tume huru ya uchaguzi, wanachama wa chama hicho wajiandae na chaguzi na wenye nia ya kugombea uongozi kuanzia Serikali za vijiji hadi mitaa waanze kujitokeza ili wajulikane.

Kauli ya Mbowe

Naye Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliyeongoza uzinduzi wa mikutano hiyo alisema Tanzania inahitaji Katiba bora, akimtaka Rais Samia kutodanganywa na mtu yeyote kwamba kuna njia ya kuondoka katika kufanikisha mchakato huo, bali lazima kuwepo kwa maridhiano.

“Katiba ya nchi yetu na Tume huru ya uchaguzi ili tusirudi tena katika zile chaguzi za…Tunataka yeyote atakayekwenda kinyume katika kuhujumu uchaguzi lazima awajibishwe. Tutakwenda katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu pale ambapo tunaamini sheria zitasimama kwenye haki.


“ Pia sheria zitasimama kwa wanaostahili na hazitamkandamiza yeyote ili kwa pamoja kulijenga Taifa salama na lenye maridhiano, litakalojenga kesho ya watoto wetu iliyobora zaidi,” alisema Mbowe, ambaye ni mbunge wa zamani wa Hai mkoani Kilimanjaro.

Katika mkutano huo, Mbowe alisema Chadema wanataka kila Mtanzania aishi kwa amani na haki itawale.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad