Rais wa Rwanda Paul Kagame
RAIS wa Rwanda, Paul Kagame amesema kwamba kundi la waasi la Democratic Forces for Liberation of Rwanda – FDLR, linaloshutumiwa na serikali ya Rwanda kwa kusababisha mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, linaungwa mkono na baadhi ya watu kwa lengo la kuipindua serikali yake. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa … (endelea).
Bila ya kutaja majina ya nchi au watu anaodai kwamba wanaliunga mkono kundi la FDLR, Kagame amedai kwamba kundi hilo linajificha katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.
Kagame amesema hayo wakati akiwahutubia maseneta. Video ya hotuba hiyo imewekwa kwenye akaunti rasmi ya You Tube, ya rais Kagame – Paul Kagame.
“Kundi la FDLR ambalo limepewa hifadhi kwa miongo kadhaa. Nadhani limehifadhiwa makusudi. Kwa FDLR na makundi mengine yenye ushirikiano nalo kuwa huko (DRC) kwa miongo kadhaa, haiwezi kuwa bila sababu maalum, haiwezekani,” amesema Rais Kagame.
“Unaposema kwamba waasi wa M23 na watu wengine ambao unawaondoa – ukisema warudi Rwanda kwa hiari au bila hiari, lakini huzungumzii kuhusu kundi la FDLR kwa sababu unalitaka kuendelea kuwepo…hiki ndio kiini cha mzozo,” ameongezea kusema Kagame.
“Huo ndio utakaso unaozungumziwa. Unataka kuliondoa kundi moja na kuliacha lingine unalopendelea. Lakini kitu kingine ni kwamba FDLR na makundi mengine unayoyasikia yanafanya hizi kelele zote. Kuna watu wanadhani kwamba wanajaribu kutafuta mbinu mbadala tofauti na ilivyo Rwanda.”
Kundi la FDLR linajumuisha waliokuwa wanajeshi wa serikali ya Rwanda, iliyokuwa madarakani kabla ya kupinduliwa na waasi wa RPF lililoongozwa na Rais Paul Kagame, mwaka 1994.
FDLR, wengi wao kutoka kabila la wahutu wanashutumiwa kwa kusababisha mauaji ya Watutsi Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Ripoti ya wataalam wa Umoja wa Mataifa kuhusu vita vya Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, inasema kwamba waasi wa FDLR wanashirikiana na jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kushirikiana kupigana na waasi wa kundi la M23.
Ripoti hiyo pia inasema kwamba Rwanda inawaunga mkono waasi wa M23, madai ambayo serikali ya Kigali imekanusha mara kadhaa.
Serikali ya Rwanda imewashutumu waasi wa FDLR kwa kuvuka mpaka na kusababisha mashambulizi ndani ya Rwanda, na kupelekea vifo vya raia.
Rais Kagame amedai kwamba kuna watu wenye nia ya kutekeleza mapinduzi nchini Rwanda.