Kajala Masanja ni muigizaji mkongwe wa filamu nchini Tanzania ambaye ameonesha mahaba mazito kwa mwanaume aliyemtambulisha kama ‘bestie’ wake.
Kajala ambaye ni mchumba mstaafu wa staa wa muziki wa Kizazi Kipya nchini Tanzania, Harmonize alimkumbusha jamaa huyo aitwaye Junior Sniper kuhusu umuhimu wake mkubwa katika maisha yake.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Kajala au Mama Paula ameposti video akiwa na jamaa huyo na kumuandikia; “Bega langu la kulilia, bestie wangu, fahamu tu kwamba wewe ni muhimu sana kwa mimi na nakupenda mpaka nakupenda tena.”
Katika video hiyo, Kajala na rafiki yake huyo wanaonekana wakinengua viuno na kushiriki wakati mzuri pamoja katika eneo la burudani ambapo muziki wa sauti ya juu ulikuwa ukipigwa.
Haya yanajiri siku moja tu baada ya muigizaji huyo mwenye umri wa miaka 40 kudokeza mpango wa kupata mtoto mwingine.
Katika yake ya Jumapili, mama huyo wa binti mmoja alidai sasa ni wakati mwafaka wa yeye kupata mwingine.
“Nadhani sasa ni muda sahihi wa kupata mdogo wako dada Pau (Paula)," aliandika kwenye Instastori yake.
Ujumbe huo ulionekana kuelekezwa kwa binti yake wa pekee, Paula Paul ambaye alimleta duniani takriban miongo miwili iliyopita.
Meneja huyo wa zamani wa Konde Music Worldwide zaidi alifichua kwamba hatatumia tena dawa za kuzuia mimba kuendelea almaarufu P2.
"Hakuna kutumia P2 tena, niko tayari kuwa mama tena," alisema.
Kajala hata hivyo, hakufichua kama tayari yuko kwenye mahusiano mengine baada ya kumtema Harmonize mwishoni mwa mwaka jana.
Kajala alitangaza kutengana na Harmonize mwezi Desemba baada ya kuwa kwenye mahusiano kwa takriban miezi minane. Wawili hao walikuwa wamerudiana mwezi Mei, 2022 baada ya Harmonize kuomba msamaha.