KOCHA Msaidizi wa Simba, Juma Mgunda, amesema ameshaandaa mafaili ya tathmini ya kikosi cha timu hiyo pamoja na michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara na tayari kwa kumkabidhi bosi wao mpya, Robertinho Oliver.
Simba ilimtambulisha Kocha Mkuu, Robertinho juzi ambaye amesaini mkataba wa miaka miwili na jioni ya siku hiyo kawasili visiwani Zanzibar, ambapo usiku alishuhudia timu yake hiyo ikishushiwa kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Mlandege FC kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi inayoendelea katika Uwanja wa Amaan.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mgunda alisema amepewa taarifa juu ya ujio wa bosi wao huyo mpya na tayari ameandaa mafaili ya tathmini ya kikosi cha Simba katika michezo 19 iliyopita na ijayo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Alisema benchi lake la ufundi wanamkaribisha kocha huyo na watatoa ushirikiano mkubwa katika kupiga kazi kwa lengo moja tu ambalo ni kufikia yanayotarajiwa na Wanasimba.
"Nifahamu ujio wa Kocha Mkuu ('Robertinho), kwa sasa sina neno juu ya uwezo wake ila natambua ni kocha mwenye uwezo mkubwa na tayari nimeshaandaa faili kwa ajili ya kumkabidhi bosi wangu ili kuanza kufanyia kazi rasmi," alisema Mgunda.
Kuhusu kupoteza mechi ya kwanza ya Kombe la Mapinduzi, Mgunda alisema yote hayo ni sehemu ya mchezo wa mpira wa miguu ambapo ukifanya makosa unaadhibiwa.
Alisema walitengeneza nafasi wakashindwa kuzitumia na wapinzani wao (Mlandege), walipata nafasi moja na kuitumia kwa kufunga bao la ushindi na kusonga mbele katika hatua ya nusu fainali.
"Kila kitu kimeonekana wazi, viwango vilivyoonyeshwa na mapungufu ya wachezaji wangu tumeyaona na jopo letu la makocha tunaenda kufanyia kazi ili kujipanga kwa mechi ijayo.
Hii mechi nimewatumia wachezaji ambao hawapati nafasi ya kucheza mara kwa mara ndani ya timu yetu ili kuwapa nafasi ya kuonyesha uwezo wao, kwa sababu hatuwezi kuwahukumu wakati hatukuwapa nafasi," alisema Mgunda.
Kikosi cha Simba leo kitakuwa na kibarua kingine katika mchezo wa pili wa mashindano hayo ya Mapinduzi kikivaana na KVZ inayonolewa na aliyewahi kuwa mchezaji na Kocha Msaidizi wa Wekundu wa Msimbazi hao, Amri Saidi.