Kocha Nabi Aweka Rekodi Mpya Yanga Aziacha Mbali Simba Na Azam



BAADA ya kikosi cha Yanga chini ya Kocha Nasreddine Nabi kugotea kwenye mechi 49 mfululizo kucheza bila kupoteza katika Ligi Kuu Bara, kasi yao imekuwa ni moto wa kuotea mbali kwa kushusha dozi kila wanayekutana naye, huku ikiaziacha mbali Simba na Azam.


Ikumbukwe kwamba, Novemba 29, 2022 kwenye Uwanja wa Highland ubao uliposoma Ihefu 2-1 Yanga, siku hiyo rekodi ya Yanga ilitibuliwa baada ya kucheza mechi 49 mfululizo za ligi bila ya kupoteza.


Mpango kazi wa Kocha Nabi kwenye mechi zilizofuata baada ya hapo ilikuwa ni mwendo wa ushindi kwa kuwa hawajapoteza wala kupata sare kwenye mechi 8 mfululizo ambazo ni sawa na dakika 720, ikiwa inasakwa rekodi mpya.


Katika msako wa pointi 24 kwenye mechi hizo nane, Yanga wamezikomba zote, huku wakifunga mabao 15 na kuruhusu 2. Ikikusanya clean sheet saba. Hivi sasa wamebakiwa na mechi tisa kumaliza msimu huu, ambapo wakishinda saba mfululizo, wanatetea taji lao.


Simba ambayo kwa sasa inanolewa na Roberto Oliveira ‘Robertinho’ wenyewe katika mechi nane zilizopita, imeshinda saba na sare moja ikikusanya pointi 22 kati ya 24. Imefunga mabao 26 na kuruhusu 6. Imeambulia clean sheet tatu.


Katika mechi hizo nane, sita ziliongozwa na Juma Mgunda, huku Robertinho akiongoza mbili ambazo zote ameshinda, hivyo ana kazi kubwa ya kufanya kushinda zote tisa zijazo kuifukuzia rekodi ya Nabi.


Azam FC imefungwa mechi mbili, sare mbili na kushinda nne, ikiambulia pointi 14 kati ya 24, hivyo imepoteza pointi kumi. Imefunga mabao 18 na kuruhusu 10. Imeambulia clean sheet mbili.


Katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, Yanga inaongoza ikiwa na alama 56, inafuatia Simba (50) na Azam (43), zote zikicheza mechi 21, bado tisa kumaliza msimu huu.


Matokeo ya mechi hizo nane ambazo Yanga ilicheza ili kuwa namna hii; Yanga 1-0 Ruvu Shootig, Yanga 1-0 Ihefu, Mtibwa Sugar 0-1 Yanga, Azam FC 2-3 Yanga, Yanga 3-0 Coastal Union, Yanga 3-0 Polisi Tanzania, Namungo 0-2 Yanga na Yanga 1-0 Tanzania Prisons.


Mechi nane zilizopita za Ligi Kuu Bara ilizocheza Simba ni; Dodoma Jiji 0-1 Simba, Simba 3-2 Mbeya City, Simba 7-1 Tanzania Prisons, KMC 1-3 Simba, Kagera Sugar 1-1 Simba, Geita Gold 0-5 Simba, Coastal Union 0-3 Simba na Polisi Tanzania 1-3 Simba.


Kwa upande wa Azam FC, ipo hivi; Singida Big Stars 1-0 Azam FC, Azam FC 3-0 Tanzania Prisons, Azam FC 6-1 Mbeya City, Azam FC 2-3 Yanga, Geita Gold 1-1 Azam FC, Kagera Sugar 2-2 Azam FC, Polisi Tanzania 0-1 Azam FC na Azam FC 3-2 Coastal Union.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad