Kurejea kwa Tundu Lissu Tanzania na ushawishi wake utaisadia vipi Chadema?



Baada ya takribani miaka mitano nje ya nchi, hatimaye mwanasiasa wa upinzani, Mbunge wa zamani wa Singida Mashariki na mwanasheria nguli, aliyepata kuwa rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Tundu Antiphas Lissu, anatarajiwa kuwasilia nchini Tanzania siku ya leo kwa mujibu wa taarifa aliyoitoa Januari 13, 2023.

“Hatuwezi kuendelea kuishi uhamishoni bila ukomo. Hivyo basi, ninapenda kuwafahamisha kwamba, panapo majaliwa, nitakanyaga udongo wa ardhi ya Tanzania kwa mara nyingine tena siku ya Jumatano ya tarehe 25 Januari, 2023, majira ya saa saba na dakika 35 mchana.”

Turudi nyuma kidogo; Tundu Lissu alianza kuishi uhamishoni nchini Ubelgiji baada ya kuondoka Kenya, Januari 2018 alipokuwa akipatiwa matibabu. Ni baada ya kunusurika shambulio la mauaji Septemba 7, 2017, katikati mwa Tanzania, Dodoma. Shambulio lililomuacha na matundu 16 ya risasi.

Tangu kushambuliwa, huu sio ujio wake wa kwanza nchini Tanzania. Ila unaashiria utakuwa wa kudumu. Alirudi Tanzania kwa mara ya kwanza Julai 2020 – ili kushiriki kinyang’anyiro cha nafasi ya urais wakati wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020. Uchaguzi uliomrudisha madarakani hayati John Pombe Magufuli, kabla ya kifo chake Machi 2021.


Tundu Lissu alirudi Ubelgiji Novemba 2020 baada ya uchaguzi kuisha. Safari ya kurudi haikuwa nyepesi. Alilazimika kwanza kukimbilia ubalozi wa Ujerumani nchini Tanzania kupata hifadhi, kwa kile alichoeleza usalama wake kuwa hatarini. Na sasa anarudi tena!

w
Maelezo ya picha, Tundu Lissu alirejea Tanzania kushirki uchaguzi mwaka 2020
Tundu Lissu bado ana ushawishi?
Gazeti la kila siku la Mwananchi, liliripoti siku chache baada ya Lissu kutangaza tarehe rasmi ya kurudi Tanzania, kwamba Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kilikuwa kikifanya maandalizi ya ujio wake. Maandalizi yaliyojumuisha kuchangisha pesa ndani na nje ya nchi kwa ajili ya mapokezi na mikutano ya hadhara.

Licha ya kuwa nje ya Tanzania kwa miaka mitano na ushei, ushawishi wake katika siasa za upinzani bado ungalipo. Kwa lugha nyingine ni kusema; makovu yake ya kisiasa hayajaondosha mvuto wake wa kisiasa mbele ya wafuasi wa chama chake.


Tundu Lissu alisifika kwa ukosoaji dhidi ya serikali ya hayati Magufuli. Hata kabla ya hapo tayari alikuwa ni mwanasiasa maarufu. Harakati zake za wakati wa Magufuli zilizidi kumuweka mstari wa mbele katika siasa za upinzani.

Wakati akiwa Ubelgiji mara kwa mara alitumia mitandao ya kijamii kuzungumza na Watanzania. Pia amekuwa akishiriki mahojiano katika vyombo vya habari kwa ndani na nje. Haya yote yamesaidia pakubwa kulifanya jina na ushawishi wake yasififie katika siasa za Tanzania.

Chanzo cha picha, IKULU TANZANIA

w
Maelezo ya picha, Rais Samia alikutana na Tundu Lissu Ubelgiji
Ataisaidiaje Chadema kuelekea 2025?
Uwepo wake ni muhimu kupamba na ushawishi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), kilichokuwa kikijifaragua peke yake katika uwanja wa siasa, tangu kuanza kwa katazo la mikutano ya hadhara na maandamano mwaka 2016.

Zuio la hayati Magufuli lilitaka mikutano ihusishe wabunge na madiwani pekee katika majimbo yao huku wengine wakitakiwa kufanya mikutano ya ndani. Ambayo nayo mara kwa mara ilikuwa ikizuiwa na vyombo vya usalama.


Lissu ikiwa ataamua kuziongoza siasa za Chadema, atakuwa na kazi ya kuhimiza kupatikana kwa katiba mpya kabla ya uchaguzi mkuu 2025. Chadema inaiona katiba mpya ni muhimu mno, kwani italinda kile watakacho kipata katika uchaguzi huo.

Ikiwa Chadema inataka kuendelea kuwa chama kikuu cha upinzani Tanzania Bara, ushawishi wa ACT Wazalendo unaozidi kukuwa kila uchao sio kitu cha kukidharau. Historia ya vyama vya upinzani Tanzania inaonesha, chama kikuu cha upinzani kinapo poromoka hakirudi tena kuwa kikuu.

w
Lissu ni mtaji na changamoto kwa Rais Samia
Mwishoni mwa mwaka 2018, Bunge La Ulaya lilikuja na dazeni ya maazimio kwa Tanzania, baada ya kile kilichoonekana kukithiri kwa ukandamizaji wa wananchi, kutokana na sheria kali dhidi ya asasi za kiraia, watetezi wa haki za binadamu, vyombo vya habari na vyama vya siasa.

Hatua hiyo iliashiria; mambo yanazidi kuharibika panapohusika uhusiano wa Tanzania na nchi nyingine hasa zile za Kimagharibi. Pia, lilikuwa ni shinikizo la kuitaka Tanzania irudi katika mstari, ama hatua kubwa zaidi zitachukuliwa.


Mabadiliko anayoendelea kuyafanya Rais Samia, ikiwemo hili la kuifanya Tanzania kuwa sehemu salama kwa wanasiasa wa upinzani na vyama vyao, yatazidi kumuongezea heshima ya uongozi wake katika majukwaa ya kimataifa.

Kurudi kwa Tundu Lissu hautokuwa mtaji muhimu tu kwa siasa za chama chake, pia utakuwa ni mtaji utakao badilisha lugha ya wakosoaji wa serikali ya Tanzania wa ndani na nje. Na katika hilo, mpokeaji mkubwa wa sifa atakuwa ni Rais Samia.  

Tundu Lissu analeta changamoto pia kwa Rais Samia. Kuruhusu mikutano ya hadhara maanake ni kuufanya uwanja wa kufanya siasa kati ya chama tawala na vya upinzani kuwa sawa. Zile zama za Chama cha Mapinduzi kusimama peke yake katika majukwaa na kunadi sera zinakwenda kufa.

Kwa kuzingatia hilo, changamoto kwa Rais Samia sasa itakuwa ni kuzidisha ushawishi wa chama chake dhidi ya vyama vya upinzani kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025. Akielewa kuwa hayuko tena peke yake katika ushindani na atamuona Lissu katika majukwaa akijaribu kuuporomosha ushawishi wake na wa CCM.

Mwezi Juni mwaka huu, serikali ya Tanzania kupitia Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, ilitoa kauli kwamba Rais Samia ametengeneza mazingira mazuri  ya kisiasa na kuifanya nchi kuwa salama, hivyo hakuna sababu ya viongozi wa kisiasa wakiwemo wa chama cha Chadema, walioko uhamishoni kutorejea nchini.


Kwa hakikisho hilo, Rais Samia atakuwa na wajibu mkubwa wa kuhakikisha usalama wa viongozi wa upinzani na wafuasi wao kama serikali yake ilivyoeleza. Itakuwa ajabu akiruhusu mikutano ya hadhara na kuahidi usalama, kisha matukio yale yale ya wakati wa hayati John Pombe Magufuli yakianza kujirudia.

Siasa za Tanzania zinachukua sura mpya. Ni ile sura iliyokuwepo kabla ya mwaka 2016 – siasa za ushindani kupitia mikutano ya hadhara. Ingawa ni mapema sana kutabiri ikiwa mambo yatabaki kuwa shuari kama yanavyoonekana kuanza.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad