Mahakama yakubali ombi la Sugu, Msigwa



MAHAKAMA Kuu Masjala Kuu, imetupilia mbali ombi lililowasilishwa na waliokuwa wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Joseph Mbilinyi na Peter Msigwa, wakilalamikia kifungo cha upweke, chakula na wafungwa kupekuliwa wakiwa utupu mbele za wengine.

Hata hivyo, imekubali hoja ya vitendo vya kuwalazimisha wafungwa kupima Virusi vya Ukimwi (VVU) na kutoa matokeo kwa watu watatu ni kuwakosea wafungwa haki ya utu, faragha na uhuru.

Hukumu hiyo ilitolewa hivi karibuni na jopo la majaji watatu, Jaji Elinaza Luvanda, Edwin Kakolaki na Ephery Kisanya.

Jopo hilo lilisema katika uamuzi wake waleta maombi walishindwa kutoa ushahidi wa kutosha kuthibitisha hoja nane kati ya tisa za kupinga uhalali wa Sheria ya Magereza inayohusu mwenendo wa mambo ya wafungwa wakiwa gerezani.

“Suala la kwanza tuligundua vitendo vya kuwalazimisha wafungwa kupima VVU na kutoa matokeo kwa watu watatu ni kuwakosea wafungwa haki ya utu, faragha na uhuru iliyoainishwa chini ya Ibara ya 12(2) na 1.6(1) ya Katiba, malalamiko mengine yote yametupiliwa mbali," lilisema jopo.


Wakati wa usikilizwaji wa ombi hilo, walalamikaji walilalamikia vitendo vya Jeshi la Magereza kuwapima wafungwa VVU kwa lazima wanapoingia gerezani na kutoa matokeo hadharani kitendo walichodai ni kinyume cha Katiba.

Pia waleta maombi walilalamikia upekuzi wa kihuni na usio na heshima kwa wafungwa kwa kuwavua nguo na kubaki utupu mbele ya watu wengine na kutoa jozi moja ya sare kwa wafungwa bila mavazi mbadala.

Waombaji walikuwa wakipinga msongamano gerezani na uhaba wa vifaa vya kulalia, kuwashirikisha wafungwa katika kazi bila malipo ya ujira, vifungo vya upweke kwa kunyimwa kutembelewa na utoaji wa mlo chini ya kiwango kilichopendekezwa.

Majaji hao walisema hakuna sheria inayoruhusu upekuzi huo kwa namna iliyoonyeshwa na waleta maombi kuwa wafungwa wanalazimika kuandamana wakiwa bila nguo, upekuzi usio na heshima katika miili yao, ikiwa ni pamoja na sehemu za siri, kulazimishwa kujisaidia kwenye ndoo.

"Sheria kama ilivyo, inataka kupekuliwa kwa heshima, adabu kwa kuzingatia heshima na faragha, matumizi mabaya tu ya madaraka hayafanyi kile kilichotolewa katika Sheria ya Kudumu ya Magereza kuwa kinyume cha Katiba.

"Sheria inayosimamia upekuzi wa wahalifu au wafungwa wanapoingizwa gerezani iko sawa na inatoa ulinzi wa kutosha kuhusiana na namna ya upekuzi wa heshima na staha unavyopaswa kufanywa.

"Iwapo kuna tabia za maofisa wa Magereza zinazokiuka sheria ya uendeshaji wa upekuzi, tunaona huo unaweza kushughulikiwa kiutawala," walisema majaji hao katika hukumu yao.


“Ushahidi kuhusu malalamiko ya mateso, adhabu ya kinyama au ya kudhalilishwa katika kifungo cha upweke haupo. 

"Kuhusu malalamiko ya utoaji wa chakula na mlo kwa wafungwa chini ya kiwango kilichopendekezwa, walisema wafungwa hawapatiwi matunda au mboga za majani kama sehemu ya ‘menu’ yao kuu, au mihogo, viazi kama sehemu ya kifungua kinywa, hawakutoa ushahidi wowote.

"Walalamikaji walikuwa na wajibu wa kutoa maelezo ya kutosha kwa mahakama kuchunguza uhalali wa Katiba ya sheria inayolalamikiwa.

“Haitoshi kwa walalamikaji kudai na kisha kukimbilia mahakamani kuomba itamke kifungu fulani cha sheria kuwa ni kinyume cha katiba bila ushahidi wa kuthibitisha kwamba kweli kuna uvunjifu."

Majaji hao walisema mahakama inaona kuwa katiba ni hati nzito na haiwezi kutumika katika jambo lisilo la maana.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad