Mandonga ulingoni tena 'Usiku wa Kisusio'



BONDIA wa Ngumi za Kulipwa nchini, Ismail Galiatano, anatarajia kupanda ulingoni dhidi ya Asanda Gingqi raia wa Afrika Kusini katika pambano la Kili Boxing Tours litakalofanyika Februari 25, mwaka huu mkoani Kilimanjaro huku wakisindikizwa na mwanamasumbwi mwenye maneno na mbwembwe nyingi,

 Karim Mandonga, imeelezwa.

Mandonga ambaye kwa sasa anatamba na ngumi yake anayoita 'Sugunyo', akijinasibu imetoka Ukraine kwenye mlipuko wa mabomu, atapanda ulingoni akitoka kushinda wiki iliyopita ugenini nchini Kenya kwa TKO dhidi ya Daniel Wanyonyi.

Pambano hilo la Februari 25, ambalo limepewa jina la 'Usiku wa Kisusio' limepangwa kupigwa katika Ukumbi wa YMCA ulioko Moshi mkoani Kilimanjaro.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na waandaji wa pambano hilo, Kampuni ya Peak Time Media chini ya Promota, Meja Selemani Sumunyu, imeeleza kuwa katika pambano hilo la Galiatano na Gingqi, pia bondia mwenye maneno na mbwebwe nyingi, Mandonga, anatarajiwa kupanda ulingoni.

Taarifa hiyo imewataja mabondia wengine wengi watakaopanda ulingoni usiku huo huku ikieleza kuwa bondia atakayepambana na Mandonga bado hajawekwa wazi pamoja na mpinzani wa mwanadada, Batuli Yassin.

Lakini ikaeleza kuwa bondia mkali na mwenye uzoefu wa kutosha Ramadhani Shauri atapanda ulingoni dhidi ya Mwinyi Mzengela wakati Alibaba Tarimo akitarajia kucheza na Salim Abeid.

Wengine watakaopanda ulingoni kwenye pambano hilo ni Mohamed Pesa ambaye atacheza na Iman Bariki huku Hussein Itaba akipewa Joseph Maigwisa na Shaban Ndaro akitarajiwa kuvaana na Musa Dragon wakati Kassim Hamad akifungua dimba na Gabriel Chola.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad