Mayele abanwa mapema, mastaa Ruvu waapa




BAADA ya kuzifunga timu 14 za Ligi Kuu, mastaa wa Ruvu Shooting wamesema hawatakubali kumruhusu straika wa Yanga, Fiston Mayele kupenya pale watakapokutana uwanjani Januari 23, wakisisitiza wanazitaka pointi tatu.

Mayele ambaye ni kinara wa mabao ligi kuu akifunga 15, tayari amezifunga timu zote isipokuwa Ruvu Shooting pekee na mchezo ujao utazikutanisha timu hizo katika Uwanja wa Mkapa Dar es Salaam.

Ruvu Shooting haijawa na msimu mzuri kutokana na kuwa nafasi ya 15 kwa pointi 14, huku Yanga wakiwa kileleni kwa alama 53 wakiwa na matumaini ya kutetea ubingwa wao.

Beki wa kushoto wa timu hiyo, Mpoki Mwakinyuke alisema wanafahamu mchezo huo utakuwa mgumu, lakini lazima wafie uwanjani kubaki na pointi tatu ili kujinasua mkiani.


Alisema wanamfahamu Mayele alivyo hivi sasa akizifunga timu nyingi isipokuwa wao, hivyo lazima wapambane kulinda heshima yao lakini kujiweka pazuri kwenye msimamo.

“Hatutakubali kumruhusu kupenya kwa namna yoyote, wachezaji tumekuwa na mabadiliko kwa sasa tukiazimia kila mechi inayokuja tunashinda kwa sababu hatupo pazuri,” alisema Mwakinyuke.

Kiungo wa timu hiyo, Shaban Msala alisema Mayele asitarajie mteremko na hawako tayari kupoteza mchezo huo huku akieleza kuwa kwa sasa timu imeimarika na kila mechi ni ushindi.


“Kama atatufunga ila hatasahau muziki atakaoupata, kimsingi tuko imara na mipango yetu ni kumbana asifurukute ili tubaki timu pekee bila kufungwa na yeye, tumejipanga vizuri,” alisema Msala.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad