Mazishi Yasitishwa Kisa Mwili wa Marehemu Kukosa Kichwa



Familia moja katika Kaunti ya Baringo imesusia kuzika jamaa yao hadi kichwa chake kitakapopatikana.


James Kiprop, mwenye umri wa miaka 38, anasemekana kuuawa na mwili wake uliokuwa umekatwa kichwa kutupwa katika Msitu wa Natasha, Eldama Ravine.

Kiprop aliripotiwa kutoweka mnamo Disemba 31, baada ya kufanya mkutano wa faragha na rafiki yake mwendo wa saa kumi na mbili jioni katika boma lao.


“Marehemu alitoweka kwa takriban wiki moja kabla ya mwili wake usiokuwa na kichwa kupatikana Jumamosi huku mikono yake ikiwa imekatwa na sehemu za tumbo lake zikiwa zimekatwa vipande,” alisema afisa wa polisi.


Kulingana na Kamanda wa Polisi wa kaunti hiyo Joseph Ongaya, bado hawajampata mshukiwa mkuu wa mauaji hayo na pia kupata kichwa cha marehemu.

Mwili wake umelazwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Eldama Ravine ili kuhifadhiwa na kufanyiwa uchunguzi wa maiti

Baba yake marehemu, Benson Tuwett, alisema familia hiyo kwa msaada wa wasamaria wema imetafuta kichwa hicho bila mafanikio.

Tuwett alisema mwanawe alitembelewa na swahiba wake kutoka kwa boma jirani akisema alikuwa na jambo la dharura kuzungumza na Kiprop.


“Rafiki yake alikuja nyumbani kwetu tulipokuwa tukinywa chai na akaomba afanye mazungumzo ya faragha na Kiprop. Walitoka nje na tangu wakati huo hatujawahi kujua walizungumza nini,” baba huyo alifichua.

Rono alitembelea boma hilo siku iliyofuata na kuondoka pamoja na marehemu na walirudi jioni, na kuwa mara ya mwisho Kiprop kuonekana akiwa hai.

"Hatujui ikiwa mtoto wetu aliondoka usiku au asubuhi. Tunachojua ni kwamba mwendo wa saa tisa usiku, alienda kulala. Mamake alipoenda nyumbani kwake asubuhi kumuomba kumsaidia kukamua ng’ombe, hakuonekana,” familia hiyo ilisema.


Ni mwiko kuzika mwili bila kichwa
Polisi wameanzisha msako wa kumkamata Rono ili kusaidia katika upelelezi na kumpata muaji wa marehemu.

Huku mwili wa Kiprop ukilazwa katika chumba cha maiti, jamaa zake, marafiki na majirani wanakusanyika nyumbani kwao kumuomboleza lakini mipango ya mazishi haitaendelea hadi kichwa chake kitakapopatikana.

"Hatuwezi kumzika mtoto wetu hadi kichwa chake kipatikane, ni kinyume na utamaduni wetu,” alisema babake.

Mzee wa Kalenjin, Kipkicho Arap Mibei aliambia TUKO.co.ke kuwa katika utamaduni wa jamii hiyo ni mwiko kuzika mwili bila kichwa.

Alieleza kuwa wazee watafanya baadhi ya matambiko ambayo yatawafanya wahusika wajitokeze na kichwa na watakidondosha kwa siri karibu na boma lake.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad