Mbrazili Simba aanza na ushindi, Saido hakamatiki




MCHEZO wa Ligi Kuu Bara kati ya Simba na Mbeya City umemalizika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa wenyeji kuibuka na ushindi mnono wa jumla ya mabao 3-2.

Mabao ya Simba yamefungwa na Saidi Ntibazonkiza 'Saido' aliyefunga mawili dakika ya 11 na 49 kwa mkwaju wa penalti huku la tatu likifungwa na Pape Sakho dakika ya 56.

Mabao kwa upande wa Mbeya City yamefungwa na nyota wake, Richardson Ng'ondya dakika ya 13 na Juma Shemvuni dakika ya 78.

Zifuatazo ni dondoo muhimu za mchezo huu.


Mabao ya leo ya Saido yanamfanya nyota huyo kufikisha tisa (9) sawa na mshambuliaji mwenzake John Bocco huku kinara kwa upande wa Simba akiwa ni Moses Phiri ambaye ana 10.

Kabla ya kujiunga na Simba, Saido tayari alishafunga mabao manne akiitumikia Geita Gold na tangu amejiunga na Simba dirisha dogo amefunga matano ikiwemo na Hat-Trick moja.

Bao la Sakho linamfanya nyota huyo kufikisha mabao sita msimu huu katika Ligi Kuu Bara huku kwa upande wa Ng'ondya linakuwa ni bao lake la tatu hadi sasa akiwa na kikosi cha Mbeya City.


Penalti ya Saido inakuwa ni ya 39 kupigwa hadi sasa katika Ligi Kuu Bara ambapo kati ya hizo ni 13 tu ambazo zimekoswa huku Dodoma Jiji ikiwa kinara kwa mastaa wake kukosa kwani katika tano walizopiga wamepata moja tu.

Kadi nyekundu aliyopewa, Samson Madeleke ni ya 21 hadi sasa kwenye Ligi Kuu Bara ambapo vinara ni Polisi Tanzania ambao wachezaji wake watano wamepata kati ya hizo msimu huu.

Huu ni mchezo wa 20 kwa timu hizi kukutana katika Ligi Kuu Bara tangu Mbeya City ilipopanda rasmi msimu wa 2012/2013 ambapo kati ya hiyo Simba imeshinda mechi 13, sare minne na kupoteza mara tatu tu katika kipindi hicho chote.

Katika michezo hiyo Simba imefunga jumla ya mabao 37 huku kwa upande wa Mbeya City wao safu yake ya ushambuliaji imefunga 15 tu.


Mchezo wa raundi ya kwanza baina ya timu hizi uliopigwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya Novemba 23, mwaka jana zilifungana bao 1-1, Simba ikitangulia kupata bao kupitia kwa, Mzamiru Yassin dakika ya 15 kisha Tariq Seif akaisawazishia Mbeya City dakika ya 78.

Mchezo wa mwisho uliopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa baina ya timu hizi Simba ilishinda mabao 3-0, yaliyofungwa na Pape Sakho aliyefunga mawili huku lingine likifungwa na Peter Banda katika mechi iliyopigwa Juni 16 mwaka jana.

Simba imeendeleza rekodi nzuri inapocheza uwanja wa nyumbani kwani tangu mara ya mwisho ilipofungwa na Yanga bao 1-0 Julai 3, 2021, imecheza michezo 26 mfululizo bila ya kupoteza ambapo kati ya hiyo imeshinda 23 na kutoa sare mitatu.

Katika michezo hiyo safu ya ushambuliaji ya Simba imeonekana tishio kwa wapinzani wake kwani imefunga jumla ya mabao 60 huku kwa upande wao wakiruhusu nyavu zao kutikiswa mara tisa tu.


Kwa upande wa Mbeya City imeendeleza rekodi mbovu inapocheza ugenini ambapo katika michezo 26 iliyopita mfululizo imeshinda mitatu tu, sare 12 na kupoteza 11 huku safu yake ya ushambuliaji ikifunga jumla ya mabao 21 wakati kwenye eneo la ulinzi limeruhusu 42.

Huu ni mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Bara kwa Kocha Mkuu wa Simba Mbrazili, Roberto Oliviera 'Robertinho' kukiongoza kikosi hicho tangu alipoteuliwa rasmi Januari 3, mwaka huu baada ya kuachana na mabingwa wa Ligi Kuu ya Uganda, Vipers.

Kabla ya Robertinho kuchukua kikosi hiki, Juma Mgunda ambaye amekabidhiwa jukumu la kuwa msaidizi wake kwa sasa alikiongoza katika michezo 16 ya Ligi Kuu Bara ambapo kati ya hiyo alishinda 11, sare minne na kupoteza mmoja tu ambao ni kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Azam FC, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Oktoba 27, mwaka jana.

Mbeya City imecheza michezo 11 mfululizo bila ya kupata ushindi tangu mara ya mwisho ilipoifunga Namungo mabao 2-1, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya Novemba 4 mwaka jana.

Timu pekee inayoongoza kwa kucheza michezo mingi bila ya ushindi ni Ruvu Shooting ambayo imecheza mechi 15 mfululizo tangu mara ya mwisho iliposhinda mabao 2-1 dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Uhuru Septemba 29 mwaka jana.


Katika michezo 20 iliyocheza Simba imeshinda 14, sare mitano na kupoteza mmoja tu ikishika nafasi ya pili na pointi 47 nyuma ya Yanga iliyopo kileleni na pointi 53.

Kwa upande wa Mbeya City katika michezo 20 ambayo imecheza imeshinda minne, sare tisa na kupoteza saba ikiwa nafasi ya 10 na pointi 21.




Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad