Mbrazili,Chama kazi ipo...Saido aingilia



JUZI Simba imeichapa Mbeya City mabao 3-2 kwenye muendelezo wa Ligi Kuu Bara lakini mjadala mkubwa ni namna kocha mpya wa Wanamsimbazi hao, Oliviera Roberto 'Robertinho' alivyomfanyia mabadiliko ya mapema staa wa timu hiyo, Clatous Chama dakika ya 33 na kuzua taharuki kwa mashabiki na wadau wa soka nchini.

Kitendo cha kumtoa Chama kilionekana kumshtua kila mmoja na kuzua taharuki kubwa sana kwa mashabiki kwa kuwa yeye ndiye staa wa timu hiyo msimu huu akiwa na asisti 12 na mabao matatu katika michezo 16 msimu huu.

Katika mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Robertinho ikiwa ni mechi yake ya kwanza ya kimashindano kuiongoza Simba, aliwaanzisha Chama, Said Ntibazonkiza 'Saido', John Bocco na Habib Kyombo kwenye eneo la mbele na kuonekana kucheza kwa maelewano makubwa ikiwemo kupata bao la kwanza ambalo Chama alimsetia Saido na kupiga kiufundi mpira uliozama nyavuni kwa Mbeya City dakika ya 11.

Muunganiko huo uliwafanya mashabiki kufurahia na kuangusha shangwe kwa kocha Robertinho lakini ghafla dakika ya 33 mambo yalibadilika baada ya kocha huyo kufanya mabadiliko mawili akimtoa Bocco aliyeumia na Chama aliyekuwa mzima na kuwaingiza Pape Sakho na Kibu Denis.


Mabadiliko ya Bocco yalipokelewa freshi kwani aliomba yeye kutolewa baada ya kuumia lakini lile la Chama likazua taharuki kuanzia kwa wachezaji wenyewe benchi la ufundi hadi mashabiki jukwani.

Kibu aliingia kuchukua nafasi ya Bocco na muda huo Sakho alikuwa anasubiri kuona nani anatoka ili aingie ndipo akaona kibao kinaonyesha namba 17 anayovaa chama na hapo hapo Sakho akaonekana kushika kichwa huku mashabiki jukwaani wakipiga kelele la kuzomea na kuanza kutupa chupa za maji kwa kocha huyo licha ya kwamba walinzi wa uwanjani walizidhibiti huku benchi la timu hiyo likiwa limeloa.

Chama alitoka uwanjani akiwa amekasirika na alivyofika kwenye benchi hakumpa mkono mtu yeyote akiwemo kocha msaidizi wa timu hiyo Juma Mgunda lakini pia hakukaa pale kwenye benchi na kupitiliza vyumba vya kubadilishia nguo lakini wakati anatoka aliona presha kubwa ya mashabiki na kuonyesha ishara ya kurudi na kweli baada ya muda kidogo alirejea na kukaa karibu na Bocco na kuanza kupiga stori.


"Tulifunga wakasawazisha na kuanza kumiliki mpira kwa kiasi kikubwa, nikaona tunahitaji wachezaji wenye kasi zaidi ili tupate bao haraka na ukizingatia tulianza mechi bila winga yeyote ndipo nikaamua kumtoa Chama ambaye kwangu hakuwa bora na kumuingiza Sakho na kama ulivyoona alileta mabadiliko," alisema Robertinho aliyetua Simba akitokea Vipers ya Uganda na kuongeza;

"Sina shida yeyote na Chama, ni mchezaji mzuri na namtegemea sana ndani ya kikosi changu, nadhani ilihitajika kuwa vile kwani nilitaka tucheze kwa kasi zaidi ambayo Chama hakuwa nayo ili kushinda mbinu za mpinzani wetu ilikuwa lazima nifanye vile."

Pamoja na maelezo hayo, Robertinho pia alisema anaitengeneza Simba kuwa timu bora ambayo itacheza kwa kasi na lengo kuu lao kwenye kila mchezo ni kushinda.
"Katika ufundishaji wangu nazingatia vitu viwili, moja ni timu kupata ushindi na mbili ni kucheza vizuri hivyo nitahakikisha Simba inakuwa katika misingi hiyo na kufikia malengo."

Alipotafutwa Chama ili kuzungumzia jambo hilo wakati anaondoka uwanjani hapo alisema maneno machache tu; "Ni mambo ya kawaida tu,  siwezi kuyazungumzia."
Kutoka kwa Chama kuliwavuruga hadi wachezaji waliokuwa ndani akiwemo Saido aliyemfuata kocha Robertinho kuanza kumuuliza imekuwaje lakini alimtuliza na kumwambia arejee uwanjani na soka kuzidi kutandazwa.


Katika mechi hiyo, Saido aliibuka nyota baada ya kufunga mabao mawili, la kwanza kwa shuti kali na la pili kwa mkwaju wa penalti huku la tatu likifungwa na Sakho kwa shuti kali wakati yale ya Mbeya City yakiwekwa nyavuni na Richardson Ng'ondya na Juma Shemvuni.
 

Wasikie wadau

Nyota wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa alisema mashabiki wa timu hiyo wanapaswa kupokea hicho ambacho kinatokea kwenye kikosi chao kwani mara nyingi kocha mpya huwa na falsafa zake hivyo inaweza kuchukua mechi tatu hadi nne kuona kiwango kizuri cha timu yao kikirejea.

"Nimeona kuwa kocha anapenda soka la kushambulia kwa kasi, mashabiki wanatakiwa kumpa sapoti kwani anaweza kutengeneza timu ambayo itakuwa tishio, anahitaji muda ili wachezaji wafiti kwenye falsafa zake, kilichotokea kwa Chama ni kawaida kwenye mpira, siku huwa hazifanani,"

"Watu wanaweza kuwa wanaona Kibu na Kyombo wakipewa nafasi, wanashindwa kuelewa kuwa mpira ni mchezo wa maelekezo, nina hakika utekelezaji wao na maelekezo ya kocha ni mkubwa, naamini kuwa huyo kocha ni bora na mashabiki wanaweza kukubaliana na hili baada ya kila kitu kuwa sawa," alisema.


Upande wake, Sekilojo Chambua alisema, "Zoezi la kujenga timu haliwezi kuwa la siku moja, kwa kiasi fulani inawekana kuwa kocha alipata mwanga kwa wachezaji wake walipokuwa kwenye kambi ya Dubai lakini bado ana kazi kubwa mbele yake kuhakikisha timu inakuwa kwenye kiwango bora, tumpe muda."

Mchezo unaofuata Simba mwenye pointi 44 katika nafasi ya pili itacheza Jumapili ya kesho kutwa na Dodoma Jiji ugenini kwenye Uwanja wa Jamhuri.
 

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad