Metacha Kurudi Yanga...Filamu Nzima ilikuwa na Wahusika Hawa, CAF Watajwa

  


Yanga Jumapili Januari 15 katika dakika za jioni kabisa kabla ya dirisha dogo la usajili kufungwa ilimrudisha kundini aliyekuwa kipa wake, Metacha Mnata kwa mkopo wa miezi sita akitokea Singida Big Stars lakini stori ya kusisimua zaidi ni namna picha hilo lilivyofanyika haraka na Mwanaspoti kujua kila kitu kilivyoenda.

Iko hivi, kabla ya juzi, Yanga haikuwa kabisa na mpango wa kusajili kipa mpya kwenye dirisha dogo la usajili lakini ripoti ya daktari waliyoipata uongozi na benchi la ufundi chini ya kocha Nassredine Nabi Jumapili jioni ikieleza kipa namba mbili wa kikosi hicho, Aboutwalib Mshery ameumia na anaweza kukaa nje ya uwanja kwa kipindi cha miezi miwili hadi sita, ikavuruga kila kitu na Wanajangwani hao fasta ikiwa kama saa 2:00 za usiku hivi yakiwa yamebaki masaa mawili kufungwa kwa usajili, wakaingia sokoni kutafuta kipa atakayesaidiana na Djigui Diarra na Eric Johora.

Kutokana na namna Metacha alivyoondoka Yanga akiwa na makosa ya kinidhamu, viongozi wa timu hiyo hawakumfikiria yeye kama chaguo la kwanza kwani waliamini kuna mashabiki hawatakuwa na imani na furaha naye licha ya kwamba aliomba msamaha lakini iliwabidi kutafuta makipa wengine na baada ya kuwakosa ikawalazimu warudi kwa Metacha.

Pendekezo la kwanza kwa Yanga ilikuwa kipa wake wa zamani, Deogratius Munishi ‘Dida’ kutokana na uzoefu wake wakiamini atashirikiana vyema na Diarra lakini timu ya nyanda huyo ya sasa, Namungo ikagoma kumuachia kwani ina mipango naye na hapo hapo Yanga ikamtaka aliyekuwa kipa wa Azam, Mzanzibar Ahmed Salula, lakini pia ikamkosa kutokana na yeye kuwa katika mafaili ya timu nyingine tayari.

Wakati presha ikiendelea kuwa kubwa kwa uongozi, mmoja wao alikumbuka ubora wa kipa wa Tanzania Prisons, Hussein Abel na wakamcheki hapo hapo lakini akawajibu kuwa tayari amesaini kuitumikia KMC hali ikazidi kuwa ngumu ndipo moja ya wajumbe akapendekeza jina la kipa wa KMKM ya Zanzibar, Nassor A Nassor lakini wakakumbuka alicheza michuano ya CAF msimu huu, hivyo asingewasaidia kwenye Kombe la Shirikisho Afrika na kuachana naye.

Baada ya hapo viongozi wa Yanga waliangalia makipa wengine bora ambao wanaweza kuwapata kwenye dakika zile za lala salama lakini wakakosa ndipo waakaamua kuwafuata Singida na kuwaomba Metacha kwa mkopo wa miezi sita na Walima Alizeti wale wakakunjua roho na kuamua kuwaachia Metacha kwa mkopo wa miezi sita na kwa haraka sana, Yanga ikamuita ofisini usiku ule kwani alikuwa Dar es Salaam na kumalizana naye usiku dakika chache kabla ya usajili kufungwa.

Hata hivyo, baada ya kutua Yanga kwa mara nyingine tena, Metacha kabla ya kufanya kitu chochote ameomba msamaha kwa wachezaji wenzake, benchi la ufundi, uongozi na mashabiki kwa kile kilichotokea hapo nyuma.

“Nimefurahi kurudi kwenye timu yangu niipendayo Yanga, hapo nyuma nilifanya makosa na nakiri, naomba mnisamehe na mnipokee. Metacha wa sasa sio yule wa nyuma, nitapambana kwa moyo mmoja na kuhakikisha timu inafikia mafanikio,” alisema Metacha.

Wachezaji wengine waliosajiliwa na Yanga kwenye dirisha dogo ni kiungo Mudathir Yahya, Beki Mmali Mamadou Doumbia, na mshambuliaji Mzambia, Kennedy Musonda.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad