MTENDAJI wa Kijiji cha Mbigili wilayani Kilosa, Briton Mshani, amefukuzwa kazi kwa tuhuma za kufanya mapenzi ofisini, pamoja na kumhonga mpenzi wake kiasi cha Sh. 1 milioni, ambazo ni fedha zilizokuwa katika akaunti ya Serikali. Anaripoti Mwandishi Wetu, Morogoro … (endelea).
Akizungumza katika mkutano na wananchi wa Kilosa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Fatma Mwasa, amesema kwamba Mshani amefukuzwa kazi baada ya baadhi ya wananchi wa kijiji hicho kumtuhumu kwa rushwa na kufanya mapenzi ofisini.
“Mtendaji wa kijiji aliyoiba fedha halafu akamhonga nyumba ndogo akageuza ofisi ya kijiji kuwa gesti, ametoa hela kwa kuhamisha akaunti ya Serikali kwenda kwenye akaunti binafsi ya mwanamke wake, huyu ameshafukuzwa kazi,” amesema Mwasa.
Katika hatua nyingine, Mwasa ameagiza mtendaji huyo wa kijiji achukuliwe hatua za kisheria huku akiagiza mtu mwingine atafutwe kwa ajili ya kujaza nafasi yake.
Mbali na tuhuma hizo, Mshani alituhumiwa kuchukua fedha za wanakijiji kiasi cha Sh. 500,000 kwa ajili ya kuwasaidia kutatua mgogoro wa ardhi, hata hivyo alikanusha madai hayo.