Mtu wa mpira: Uchaguzi Simba bado umekaa kizamani



Nyakati zinakwenda kasi sana lakini bahati mbaya kuna vitu vimebaki kizamani zamani. Ni kama hii klabu ya Simba. Bado ipo kwenye zama za mawe.


Leo Simba itafanya Uchaguzi Mkuu wa viongozi wake kwa upande wa Wanachama. Watachagua Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi kwa upande wa Wanachama.


Katika uchaguzi huo kuna wagombea 12, wawili wanaowania Uenyekiti ambao ni Wakili Moses Kaluwa na anayetetea kiti, Murtaza Mangungu, huku wanaowania Ujumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ikiwa na watu 12, wakiwamo Asha Baraka na Pendo Aidan Mapugilo wakiwa wagombea wakike pekee wanaowania nafasi moja kwa upande wa jinsia yao.


Ikumbukwe kuwa Simba ilibadili Katiba yake miaka kadhaa iliyopita ili kuruhusu mfumo mpya wa uendeshaji ambao una kampuni ndani yake.


Ni katika mfumo huu ambao umemruhusu Mohamed Dewji kuwekeza kwa kununua asilimia 49 ya Hisa kwa Shilingi 20 Bilioni. Ndio mfumo ambao umempa Dewji mamlaka makubwa ndani ya klabu ya Simba.


Pamoja na upande wa Mwekezaji kuwa na asilimia ndogo ya Hisa lakini bado ndio wenye maamuzi makubwa kulingana na Katiba ya Simba. Inashangaza sana, lakini hakuna anayehoji. Ila kwa sasa tuachane na hilo kwanza. Turudi kwenye uchaguzi.


Tumeona namna mchakato mzima umekwenda. Bado kumekuwa na malalamiko ya mizenge na rafu kibao kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.


Kuna watu wanalalamikia kukatwa ‘kienyeji’. Ni kama tu ilivyokuwa zama za mawe. Watu walikatwa kwa ‘figisu’ na hakuna aliyejali.


Inashangaza kuona tupo nyakati hizi za utandawazi lakini mambo haya ndani ya klabu ya Simba yamekwenda kienyeji. Achana na hilo kwanza.


Linaloshangaza zaidi ni hili la mfumo wa wanachama. Bado Simba inatumia vitabu vya zamani. Watu wanalipa ada zao kwa stakabadhi kama zamani.


Yaani leo hii uchaguzi umefika wanachama ndio wanalipia ada zao za mwaka. Wengi wao hawa hawakuwahi kulipa ada zao tangu uchaguzi uliopita. Leo ndio wamekumbuka kuwa ni wanachama kwa sababu ya uchaguzi?


Simba bado inatunza majina ya wanachama wake katika madaftari na vitabu maarufu kama leja. Kama watu wa kale katika dunia ya kisasa.


Hawana mfumo wa kueleweka wa kidigitali. Kuna wakati fulani walianzisha mfumo wa kusajili Wanachama kupitia benki fulani. Wakati huo Senzo Mbatha alikuwa Mtendaji Mkuu. Mfumo huu ulifia wapi? Wanajua wenyewe.


Yaani miaka mingi imepita baada ya hapo. Hakuna wanachama wapya. Waliokuwepo ni wale wale. Kwanini? Wanajua viongozi waliokuwepo.


Kwenye hili Simba imebaki kizamani sana. Leo hii utakuta wanachama wengi wanalipiwa kadi zao na wagombea ili wakawachague. Ilikuwa hivi tangu enzi na enzi. Wakati huo kina Khamis Ng'ombo ana sauti kubwa kuliko mwenyekiti wa klabu.


Enzi hizo Daniel Kamna ana mamlaka zaidi kuliko katibu wa klabu. Ni enzi hizo Mzee Hassan Dalali 'Field Marshall' akiwa Mwenyekiiti wa Matawi ya Simba Mkoa wa Dar es Salaam na Seydou Rubeya akimtetemesha Kassim Dewji kipindi cha mpasuko wa Simba Banyamulenge, Simba Chai na Simba Taleban.


Wengi walidhani mabadiliko ya mfumo yameiweka Simba kisasa kumbe wapi. Hata kampeni bado zina ile uzamani wa kupakaziana machafu badala ya kutembeza sera ili wanachama wafanye maamuzi ya kumpa nani uongozi.


Wanachama hawalipi ada zao hadi uchaguzi ufike. Wanalipiwa na wagombea wanaotaka kura ambao wana uwezo wa kufanya hivyo. Inachekesha sana.


Hii inamaanisha mpaka leo Simba hainufaiki chochote na wanachama wake. Haijali kuhusu hazina hii zaidi ya kusubiri wakati wa uchaguzi pekee ili waje kuwachagua watu fulani fulani.


Nilidhani baada ya mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji, Simba ingekuwa na mfumo mzuri wa uendeshaji na wanachama. Tusingekuwa tunategemea huu wa stakabadhi kama vile unanunua mahindi kwa wakulima.


Angalau Yanga baada ya kubadili tu Katiba walianzisha mfumo mzuri wa kusajili wanachama kwa njia ya Mtandao. Tumeona namna ambavyo wamevuna hazina kubwa kutoka kwa wanachama wake.


Imeondoa hii tabia ya kale kwa wagombea kulipia watu ada za wanachama ili wakawachague. Imeondoka katika zama hizi za zamani.


Hii inatoa fursa kwa wagombea kumwaga sera zao zaidi kuliko kutegemea haya mambo ya kufufua uanachama wa wengine.


Simba wanakwama wapi? Wao ndio wolitangulia katika mabadiliko. Wakaonyesha nia ya kuwa na mfumo mzuri lakini mpaka leo bado haijaeleweka.


Uchaguzi wa pili huu wanakwenda katika mfumo ule ule wa kizamani. Ubaya ni kwamba hata wagombea waliopo hakuna aliyeonyesha mipango ya wazi ya kwenda kubadili mfumo huu. Ni ajabu sana.


Timu za kisasa zinapaswa kuendeshwa kisasa. Simba inapaswa kupiga hatua katika hili. Natamani baada ya hapa kuona wanakuwa na mfumo mzuri zaidi wa wanachama wake. Huu wa kizamani hauna tija.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad