Rubani mwenza wa ndege iliyoanguka Nepal siku ya Jumapili alipoteza mumewe katika ajali ya ndege miaka 16 mapema, imeibuka.
Anju Khatiwada alikuwa akiongoza ndege ya shirika la ndege la Yeti nambari 691 wakati ilipogonga korongo karibu na mji wa kitalii wa Pokhara, na kuwauwa wote waliokuwa ndani ya ndege hiyo katika maafa mabaya zaidi ya anga kuwahi kutokea katika kipindi cha miaka 30.
Mumewe Dipak Pokhrel pia alikuwa akiongoza ndege ya shirika la ndege la Yeti alipofariki – na kifo chake ndicho kilimchochea Anju kujiingiza katika taaluma ya urubani.
Akiwa amefadhaishwa na kifo chake, akiwa peke yake na mtoto wao mdogo, huzuni ya Anju ikawa nguvu yake ya kumtia moyo.
“Alikuwa mwanamke aliyedhamiria ambaye alisimamia ndoto zake na kutimiza ndoto za mumewe,” mwanafamilia Santosh Sharma alisema.
Dipak alikuwa kwenye chumba cha marubani cha ndege ya aina ya Twin Otter ambayo ilikuwa imebeba mchele na chakula kuelekea mji wa Magharibi wa Jumla iliposhuka na kuwaka moto mwezi Juni 2006, na kuua watu wote tisa waliokuwa ndani ya ndege hiyo.
Miaka minne baadaye Anju alikuwa kwenye safari ya kuwa rubani, akishinda vikwazo vingi vya kupata mafunzo nchini Marekani. Mara baada ya kuhitimu, alijiunga na Yeti Airlines.
Anju ambaye ni mtu wa kuvunja rekodi kwa kupambana na vikwazo vingi maishani , alikuwa mmoja wa wanawake sita tu walioajiriwa na shirika la ndege kama marubani, na alikuwa amesafiri kwa karibu saa 6,400.
“Alikuwa nahodha kamili katika shirika la ndege ambaye alikuwa amefanya safari za peke yake,” Sudarshan Bartaula kutoka Yeti Airlines alisema. “Alikuwa mwanamke jasiri.’
Baadaye Anju aliolewa tena na kupata mtoto wa pili huku akiendelea kujenga taaluma yake. Marafiki na familia wanasema aliipenda kazi yake, na alifurahi kuwa karibu.
Katika eneo la ajali huko Pokhara, sehemu za ndege ambayo Anju alikuwa akiiendesha pamoja, zikiwa zimetawanyika kwenye kingo za Mto Seti, zikiwa zimetapakaa kama vipande vya mwanasesere iliyovunjika. Sehemu ndogo ya ndege iliwekwa kwenye korongo, madirisha yakiwa yamebakia na rangi ya kijani na manjano ya Yeti Airlines bado inaonekana.
Mkasa wa wiki hii umezua gumzo kuhusu usalama wa mashirika ya ndege katika taifa hilo la Himalaya, ambalo limeshuhudia mamia ya watu wakifariki katika ajali za ndege katika miongo ya hivi karibuni.
Kwa miaka mingi, sababu kadhaa zimelaumiwa kwa rekodi mbaya ya usalama ya mashirika ya ndege ya Nepal. Mandhari ya mlima na hali ya hewa ambayo mara nyingi haitabiriki inaweza kuwa gumu kutabiri, na mara nyingi hutajwa kama sababu. Lakini wengine wanataja ndege zilizopitwa na wakati, kanuni zilizolegea na uangalizi mbaya kama mambo yanayochangia ajali hizo.
Bado haijafahamika ni nini kilisababisha ajali hiyo ya Jumapili.