Mwili wa aliyekuwa mfanyakazi wa TBS wazikwa chini ya ulinzi



ALIYEKUWA mfanyakazi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Henry Massawe, jana alizikwa chini ya usimamizi wa Jeshi la Polisi Pwani katika eneo alikokuwa akiishi Kiharaka, Kata ya Mapinga mkoani Pwani.

Waombolezaji, ndugu, jamaa na marafiki wakishiriki kumzika marehemu Henry Massawe nyumbani kwake Kiaraka Magengeni, Wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani jana. PICHA: ELIZABETH ZAYA
Polisi ililazimika kusimamia mazishi hayo baada ya Mahakama ya Wilaya ya Bagamoyo kuamuru mwili huo kuzikwa katika nyumba yake aliyokuwa akiishi.

Mwili huo umezikwa bila mke wa marehemu, Janeth Ikuyumba, kushiriki na mama mkwe, mtoto wake na msaidizi wa nyumbani wakiwa wamejifungia kwa ndani.

Mfanyakazi huyo wa TBS alifariki Januari 16, mwaka huu, lakini hakuzikwa baada ya kuibuka kwa mgogoro kati ya ndugu zake marehemu na mke wake.

Ndugu walisema kabla ya umauti kumfika, kijana wao alitaka azikwe nyumbani kwake Kiharaka alipokuwa akiishi, lakini mke wake alidai mumewe alitaka azikwe nyumbani kwao alikozaliwa, Moshi mkoani Kilimanjaro.


Ndugu walipomshinikiza azikwe nyumbani kwake, mke alikimbilia mahakamani kwenda kuweka zuio.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Kiharaka, Simoni Kilian, alisema uamuzi wa mahakama wa kuzikwa marehemu huyo ulitolewa jana asubuhi na kuomba ulinzi wa polisi kufanikisha mazishi hayo kwa amani.

"Huyu kijana alikuwa ni mkazi mzuri na mwema kwenye huu mtaa na hata sisi tulishangaa kwa nini hili lilitokea, lakini cha kushukuru limeisha, tumezika kwa amani. Mke wake hakushiriki na hata mama yake mzazi walijifungia  ndani na mtoto wa marehemu ambaye mi mdogo kama miaka miwili au mitatu hivi na msichana wa kazi, nafikiri walifanya hivyo kwa hofu."


"Lakini mimi niliwahakikishia kwamba hakuna lolote baya litakalowapata na kuna amani ya kutosha."

Kiliani alisema kabla ya kuingiza mwili ndani walialazimika kuvunja mlango kwa sababu ulikiwa umefungwa kwa ndani na baada ya kumaliza shughuli ya mazishi waliufunga kama walivyoukuta.

Mmoja wa kijana aliyekuwa akifanya kazi na merehemu ambaye hakupenda jina lake litajwe, alisema Henry ameugua kama wiki tatu na mara ya mwisho walikuwa naye jijini Dodoma kwenye mkutano wa kikazi wa Shirika lao katikati ya mwezi Desemba, mwaka jana.

"Tulikuwa tukiwasiliana anasema kwamba anaumwa ndiyo maana haji ofisini kwa siku chache hizo, lakini tukajua sio serious kihivyo."


"Nilichojifunza ni kwamba kuna umuhimu wa kuandika wosia pale tu unapokuwa na familia au kuwa na mali zako. Vijana wengi hatufanyi hivyo tunafikiri ni mpaka uwe mzee ndiyo uandike, hili ni funzo.”

Alisema wamebaini Henry na mkewe walikuwa na ugomvi wa muda mrefu.

"Tumekibaini kwamba hawa watu walikuwa na ugomvi wa muda mrefu yeye na mke wake, walifunga ndoa mwaka 2018, lakini inavyosemekena tayari ndoa yao ilikiwa na mgogoro mkubwa," alisema.

"Cha kushangaza Henry hakuwahi kutuambia, yaani ni bora kama angetuambia labda tungejua namna ya kumsaidia. Alikuwa ni mshikaji sana, anacheka sana na watu, mchapakazi."


Mmoja wa majirani, Lucas Mwakapeje, alisema majirani ndio walioshiriki kwa kiwango kikubwa kufanikisha mazishi hayo wakishirikiana na polisi kuvunja mlango wa geti na kuingiza mwili, kuhakikisha umezikwa na kila kitu kimekaa sawa.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad