MZEE WA UPUPU: Manara asaidie uchunguzi


Wikiendi iliyopita kupitia akaunti yake ya Instagram, Haji Manara alifichua mbinu ambazo klabu yake ya zamani, Simba SC, ilikuwa ikizifanya kupata ushindi. Kwa kujiamini kabisa, Haji ameandika Simba haiwezi kuifunga Yanga kwa sasa kwa sababu watu ambao walikuwa wakiwatumia anawajua ikiwa na maana anajua namna ya kuwadhibiti.


Pia, mbinu zao anazijua akizitaja kwa lugha ya ‘Cuba’ rushwa na dawa aina ya 4.4.2 ambayo huwachosha wachezaji. Hizi ni tuhuma nzito ambazo hazipaswi kufanyiwa masihara hata kidogo.


Kwa kuwa amethibitisha dhahiri Simba ilikuwa ikitumia mbinu wakati akifanya kazi huko, basi nadhani anatakiwa kuisaidia mamlaka kubaini hilo na kama kuna zaidi ya hilo. Hivi ndivyo mamlaka za Italia zimekuwa zikifanya kuibaini Juventus kila wakati.


Mwaka 2006 klabu hiyo ilishushwa daraja baada ya kubainika ilikuwa ikihonga waamuzi kuisaidia kupata ushindi. Kashfa hii iliyopewa jina la Calciopoli ilisababisha Mkurugenzi Mkuu wa Juventus, Luciano Moggi na mtendaji mkuu wa klabu hiyo, Antonio Giraudo kufungiwa maisha kujihusisha na soka.


ILIVYOANZA


Mwaka 2004, gazeti moja maalumu kwa ajili ya mashabiki wa klabu ya AS Roma linaloitwa Romanista, liliandika habari kuhusu tetesi za kashfa mbili kwenye mpira wa Italia. Moja iliwahusu wachezaji wa Juventus kutumia dawa za kusisimua misuli zilizopigwa marufuku michezoni na nyingine ilihusu uchezaji kamari na rushwa kwa waamuzi.


Jeshi la polisi likazipa uzito mkubwa tuhuma hizi na kuunda kikosi kazi kufanya uchunguzi. Japo uchunguzi huo haukubaini chochote kuhusu tuhuma hizo, lakini ulisababisha kubainika kwa mambo mengine makubwa zaidi ya hayo.


Ukubwa wa mambo hayo ukasababisha mahakama ya Turin kuingilia kati kufanya uchunguzi kwa kutaka kushirikiana na Shirikisho la Soka la Italia (FIG), lakini mahakama hiyo ikaja kubaini kwamba hata shirikisho hilo siyo safi...linahusika!


Serikali ya Italia chini ya Waziri Mkuu, Silvio Berlusconi, haikutaka uchunguzi uendelee kwa sababu klabu yake ya AC Milan ingeweza kukutwa na hatia pia. Kwa hiyo akaweka kigingi. Mahakama ikakosa nguvu hivyo ikavujisha kashfa hiyo kwenye vyombo vya habari, navyo vikaibatiza jina la CALCIOPOLI yaani kashfa ya soka.


Magazeti yakaandika kuhusu hilo sakata kila uchao na kusababisha hali kuwa ngumu. Wakati wa kuchunguza rushwa kwa waamuzi kwenye zile tetesi za Romanista, ilibainika kigogo wa klabu ya Juventus, Luciano Moggi alikuwa akiwasiliana moja kwa moja na mkuu wa kamati ya waamuzi ili apange waamuzi watakaoipendelea klabu hiyo.


Sauti za mazungumzo yao ya simu ambazo zilipatikana kwenye mamlaka ya mawasiliano zikawekwa hadharani na vyombo vya habari. Ilibainika wachezaji muhimu wa timu pinzani kwa Juventus walikuwa wakionyeshwa kadi za njano na nyekundu ili kudhoofisha timu zao na Juventus kutopata upinzani wa kutosha.


Japo Juventus ndiyo walikuwa vinara, lakini klabu kadhaa zilihusika na kashfa hii, ikiwemo AC Milan, klabu iliyokuwa ikimilikiwa na Waziri mkuu aliyekataa kuruhusu kufanyika kwa uchunguzi.


KWETU SASA


Kwa hiyo alichokiandika Haji kwenye Instagram yake kinaweza kutusaidia kama kile kilichoandikwa na Romanista kule Italia. Uchunguzi uanzie hapo, Haji aitwe na mamlaka. Aseme kile anachokijua zaidi ya kile alichokiandika kwenye Instagram.


Ashirikiane na mamlaka kubaini kila uchafu aliohusika nao wakati yuko Simba SC, kama alivyosema. Haiwezekani tuhuma nzito kama alizozianisha zipite pasi na uchunguzi wowote.


ALICHOANDIKA HAJI INSTAGRAM


Aliposti video ya mama mmoja akiuliza swali kwenye mkutano wa kampeni za uchaguzi wa Klabu ya Simba. Mama hiyo alikuwa akimkumbusha mwenyekiti wa klabu hiyo, Murtaza Mangungu, juu ya ahadi yake kwenye uchaguzi uliopita ya kuifunga Yanga, lakini haikutelezeka na badala yake sasa Simba inashangilia sare na Yanga.


Haji akaandika “Kumbe Makolo kutoa droo na mabingwa wa nchi wanashangilia, kwa nini huwa hamsemi? Halafu kuna mazuzu wanaojiita wachambuzi huwa wanasema eti tuwaige manyonyo, Yanga Afrika hii iige timu inayoshangilia kutoka sare na sisi?


Ila kwa hili Ngungu anaonewa aisee, pamoja na ubora wa kikosi chetu na mikakati imara ya uongozi wa Yanga, mnadhani mimi nitakubali nifungwe na Madunduka? Mbinu zao zote chafu nazijua, Watapenyea wapi wakati mimi nipo?


“Sio Ngungu wala Try Next au Mudi mwenyewe hawawezi kuifunga Yanga hii abadan, tutawapasua daily na ushindi wao ndio hiyo droo ya papatu papatu, ya Mungu nisaidie!


“Shida yao kubwa ni kutumia mbinu za kizamani ambazo mimi nazijua in and out, nimeishi nao wale na nawajua vizuri, Yanga hii haipigishwi, tuna wachezaji waaminifu mno, hivi @djiguidiarraofficial au @jobdick05 wanaanzaje kucheza michongo yao?


“4:4:2 watatufanyia sisi? Team yetu bora kuliko yao, watatufungaje sasa zaidi ya mbinu zao ambazo zimepitwa na wakati, hao wanaowaamini kuwatuma wanajua nawajua kama nimewazaa mie, dadadeki.”


Maneno haya, hasa aya mbili za mwisho zinaeleza kuwa msaada mzuri kwa mamlaka kupata pa kuanzia.


Mamlaka zisikubali hili jambo kupita hivi hivi, lazima uchunguzi ufanyike. Yawezekana Haji anayajua mengi zaidi ya haya.


Mwanaspoti

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad