WAZIRI wa Habari, Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Nape Nnauye, amewataka waandishi wa habari kufuata maadili ya kitaaluma wakati wanaripoti mikutano ya hadhara, ili kuepusha habari ambazo zinaweza kuligawa Taifa. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).
Nape ametoa wito huo hivi karibuni akizungumza na wanahabari, ikiwa ni siku chache baada ya vyama vya siasa nchini kutangaza kusudio la kuanza kufanya mikutano ya hadhara, kufuatia Rais Samia Suluhu Hassan, kuondoa zuio la mikutano hiyo lililowekwa na mtangulizi wake, Hayati John Magufuli.
“Sio kila kitu ni stori, kwa sababu tunapeleka kwa mwingine kile tunachoandika, wito wangu uhuru uliotolewa wa mikutano ya hadhara utumike vizuri, turekodi yale ambayo yana faida kwa nchi yetu. Kama kukosoa tukosoe kwa ukweli, tukabalance stori na tukumbuke tuna wajibu wa kuhakikisha taifa hili linakuwa moja likiparanganyika wanahabari hamko juu ya hili,” alisema Nape.
Waziri huyo wa habari, aliwataka waandishi wa habari kutoandika maudhui yenye matusi, pamoja na kusikiliza pande zote mbili katika masuala yenye tuhuma ama madai (ku-balance stori).
“Tendeni haki kwenye stori zenu, msionee mtu m-balance stori zitakazotokana na mikutano sababu tukibeba hivi tunaweza kuwapelekea watu kusiko na situ ku-balance lakini hakuna sababu ya kuchapisha matusi kama mtu umeenda mahali ametukana huyo muache atukane ondoka zao au toa neno zuri alilotoa,” alisema Nape.
Aidha, Nape alimshukuru Rais Samia kwa kuimarisha uhuru wa habari “ameongeza uhuru kwenye tasnia ya habari nadhani kuliko wakati wowote katika historia, sikumbuki toka nimekuja hatujakamata na wala hatujamfinya mtu. Ukikosea tutakutafuta tukushauri. Tumewapa uhuru lengo lake mtusaidie kuwa macho kuhakikisha rasilimali za nchi yetu zinafaidisha wengi.”
Katika hatua nyingine, Nape alisema wizara yake inafanyia kazi agizo la Rais Samia la kuzifanyia marekebisho sera zinazosimamia tasnia ya habari.