Washambuliaji wasiojulikana wamechoma moto makazi ya mhubiri wa kanisa Katoliki kaskazini magharibi mwa Nigeria. Wakati wa shambulizi hilo, mhubiri mmoja alichomwa moto mgongoni akiwa hai hadi kufa, na mwingine alipigwa risasi na kujeruhiwa alipojaribu kukimbia.
Kasisi aliyenusurika alikimbizwa hospitalini kwa matibabu. Sababu za shambulizi hilo bado haijajulikana.Saa chache baadaye, majambazi walifanya shambulizi jingine tofauti katika jimbo la Katsina, kaskazini mwa nchi hiyo.
Katika tukio hilo, mhubiri alipigwa risasi na wengine watano walitekwa nyara, walipokuwa wakijiandaa kuhudhuria ibada ya Jumapili. Eneo la kaskazini mwa Nigeria lina wanamgambo wengi wenye misimamo mikali ya dini ya Kiislamu, ambao wamekuwa wakifanya machafuko ikiwemo utekaji nyara.
Machafuko hayo yamezidisha wasiwasi kwamba huenda uchaguzi wa rais ambao umepangwa Februari 25, hautafanyika katika baadhi ya maeneo.