Ndege iliyokuwa na watu 72 imeanguka karibu na uwanja wa ndege katikati mwa Nepal na takriban miili 40 imepatikana, maafisa wanasema.
Watu wasiopungua 67 wamekufa leo Jumapili Januari 15, 2022 baada ya ndege ndogo ya abiria kuanguka kwenye mkoa wa Pokhara nchini Nepal.
Mamlaka ya usafiri wa anga nchini humo imesema hiyo ni ajali mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa kwenye taifa hilo la safu za milima ya Himalaya kwa karibu miaka 5 iliyopita.
Mamia ya waokoaji bado wanaendelea kupekua eneo la ajali iliyotokea kwenye korongo karibu na uwanja wa ndege wa Pokhara.
Ndege hiyo ilikuwa imewabeba watu 72 ikitokea mji mkuu wa Nepal, Kathmandu. Msemaji wa mamlaka ya usafiri wa anga Jagannath Niroula amesema wakati ajali ikitokea hali ya hewa ilikuwa nzuri.
“Miili ya watu 31 tayari imeondolewa eneo la tukio na kupelekwa hospitali” amesema Noruala alipozungumza na shirika la Habari la Reuters. “Miili mingine 36 bado ikio eneo la ajali na mipango inafanyika kupeleka Kreni kuiondoa” ameongeza.
Kituo kimoja cha televisheni nchini humo kimeonesha wafanyakazi wa uokozi wakipekua sehemu ya ndege hiyo iliyoanguka huku eneo jingine moto ukiwa bado unawake.
“Ndege inaungua”, amekaririwa akisema afisa wa polisi Ajay K.C, na kuongeza kwamba wafanyakazi wa uokozi wanapata tabu kulifikia vizuri eneo la ajali ambalo katikati mwa korongo kubwa linalopatikana Jirani na uwanja wa ndege wa mji wa Pokhara.
Miongoni mwa waliokuwemo kwenye ndege hiyo aina ya ATR chapa 72 ni pamoja na Watoto wawili na wafanyakazi 4. Abiria waliokuwemo ni raia 5 wa India, 4 wa Urusi, 1 wa Ireland, 2 kutoka Korea Kusini, na mmoja mmoja kutoka Australia, Ufaransa na Argentina.
Nepal – Flugzeugabsturz in Pokhara
Ndege hiyo ilifanya mawasiliano ya mwisho na uwanja wa ndege wa Seti Gorge saa nne asubuhi saa za Nepal na muda mfupi baadaye ilianguka.
“Nusu ya ndege hiyo iko upande wa mwinuko” amesema Arun Tamu, mkaazi wa eneo hilo, ambaye ameliambia shirika la Habari la Reuters kuwa alifika eneo la ajali dakika sita baada ya ndege kuanguka.
“Nusu nyingine ya ndege hiyo imetumbukia kwenye korongo la mto Seti” ameongeza shuhuda huyo.
Shuhuda mwingine Khum Bahadur Chhetri alitizama akiwa juu yap aa la nyumba yake wakati ndege hiyo ilipokuwa ikielekea kutua.
“Niliona ndege ikitikisika na kuyumbayumba kushoto na kulia, na ghafla ikaanguka na kutumbukia kwenye korongo” amesema Chhetri na kuongeza kwamba wakaazi wa eneo hilo walifanikiwa kuwaokoa abiria wawili na kuwakimbiza hospitali.
Uchunguzi waanzishwa kubaini chanzo cha ajali hiyo mbaya
Serikali tayari imeanzisha jopo la kuchunguza sababu ya ajali hiyo na ripoti inatarajiwa kutolewa ndani ya siku 45 zijazo. Hayo yamesema na Waziri wa fedha wa Nepal Bishnu Paudel.
Ajali hiyo ndiyo mbaya zaidi tangu mwaka 2018, wakati ndege aina ya Dash 8 kutokea mjini Dhaka, Bangladesh kuanguka ilipokuwa ikitua mjini Kathmandu na kuwaua watu 51 kati ya abiria 71 walikuwemo.
Watu wasiopungua 309 wamekufa tangu mwaka 2000 katika ajali za ndege au helikopta nchini Nepal, taifa linalofahamika kwa kuwa na milima mirefu zaidi duniani ikiwemo Mlima Evarest.
Mwaka 2013, Umoja wa Ulaya ulikwishayapiga marufuku mashirika ya ndege ya Nepal kutumia anga ya kanda hiyo kutokana na wasiwasi juu ya usalama.