Sababu Mandonga kubadilishiwa mpinzani




Karim 'Mandonga' Said amebadilishiwa mpinzani, ambapo sasa atazichapa na Daniel Wanyonyi bondia ambaye hatakuwa na cha kupoteza kama atapigwa usiku wa leo akicheza nyumbani nchini Kenya.

Mandonga atacheza na Wanyonyi ambaye hayupo 'active' kwenye ndondi, mara ya mwisho alipigwa kwa Technical Knock Out (TKO) na Abdallah Pazi (Dullah Mbabe).

Awali, Mandonga alitakiwa kuzichapa na Denzel Onyango Okoth, bondia chipukizi kwenye ngumi za kulipwa aliyepigana mapambano mawili na kushinda yote kwa TKO.

Akizungumzia sababu za Mandonga kubadilishiwa mpinzani, Rais wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC), Chaurembo Palasa amesema ni za kiufundi.


"Kwenye ngumi bondia anaweza kubadilishiwa mpinzani ndani ya saa 24," amesema Palasa.

Kwa Wanyonyi, Mandonga atakuwa na kibarua zaidi cha kuhakikisha anashinda ugenini ili kulinda renki na nyota moja aliyonayo hivi sasa.

Kama atapigwa, kuna uwezekano mkubwa wa kupoteza nusu nyota na kupiromoka kwenye ubora wa dunia ambako sasa ni wa 446 na watano nchini, rekodi ambayo aliipata baada ya kumchapa Said Mbelwa Novemba mwaka jana.


Wanyonyi tangu Februari, 2021 alipochapwa na Mbambe hajawahi kurudi ulingoni hadi leo atakapotafuta fursa ya kurudi kwenye renki kupitia kwa Mandonga.

Kama atashinda, atarudi upya kwenye renki za mtandao wa ngumi za kulipwa wa dunia (Boxrec) ambako hadi sasa hayupo 'active'.

Hata hivyo, Wanyonyi licha ya kupotea ulingoni karibu miaka miwili, bado ni mzoefu akiwa amepigana mapambano 43, aneshinda mara 27 amepigwa mara 14 na kutoka sare mara mbili.

Miongoni mwa Watanzania aliowachapa ni Karama Nyilawila kwa pointi na Jacob Maganga kwa TKO.

Akizungumzia athari za bondia  kubadilishiwa mpinzani siku chache kabla ya pambano, bingwa wa zamani wa dunia wa WBF, Francis Cheka amesema, inatokea pale bondia anapokuwa amejiandaa kucheza na mtu mwingine na kumsoma mpinzani tofauti na yule anayekwenda kupigana naye.

"Amejifua kwa ajili ya mtu mwingine, unapobadilishiwa kama hujapata muda wa kumsoma mpinzani wako, zile raundi za mwanzo anaweza kukupa tabu," amesema.

Tukio kama hilo liliwahi kumtokea Dullah Mbabe na kuchapwa kwa TKO na Tshimanga Katompa, ambaye hakuwa amepangiwa awali kucheza naye na kubadilishiwa saa chache kabla ya kupanda ulingoni

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad