Sakata la Kiungo Mshambuliaji wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Yanga Benard Morrison limeendelea kuzungumzwa na Kocha Mkuu Nasreddine Nabi.
Morrison aliondoka Yanga mwishoni mwa mwaka 2022, kuelekea nchini kwao Ghana kwa ajili ya kushughulikia masuala ya kifamilia.
Kocha Nabi amesema suala la kuondoka kwa Morrison klabuni hapo sio tatizo, kwa sababu alitumia nafasi yake kama mchezaji kwa kuomba ruhusa ya kurudi kwao kwa ajili ya masuala ya kifamilia.
Amesema suala la kuomba ruhusa kwa mchezaji ni utaratibu wa kawaida, lakini kushindwa kurejea kwa wakati kambini ndio tatizo ambalo kwake hataendelea kulifumbia macho.
“Sina tatizo na mchezaji kuomba ruhusa, hata mimi kama kocha huwa naomba ruhusa lakini unaheshimu muda wa kurejea kazini, siwezi kuwa na furaha na mchezaji ambaye hana heshima na klabu, HAKUNA staa mkubwa kuliko hii timu,” amesema Nabi
Hata hivyo, inadaiwa kuwa Morrison amechelewa kurejea kambini kwa madai ya kutofautiana na Uongozi wa Yanga, akidai sehemu ya malipo yake ya ada ya usajili ambayo alipaswa kulipwa alipojiunga na Klabu hiyo mwanzoni mwa msimu huu akitokea Simba SC.