Dar es Saalam. Kaimu Mkurugenzi wa Manispa ya Kinondoni, Jumanne Mtinangi ametolea ufafanuzi mgahawa wa Shishi Food unaomilikiwa na msanii Shilole baada ya kuvunjwa ili kupisha ujenzi wa kituo cha Afya cha Kata ya Kinondoni.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Alhamisi Januari 19, 2023 Mtinangi amesema eneo alilokuwa msanii huyo akodishiwa kwa sababu lilikuwa ni eneo la wazi ambapo kwa sasa pana zahanati ya Kinondoni.
"Eneo lile lilikuwa la wazi kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Kinondoni, Manispaa imekuwa na utaratibu wa kuwapa wananchi maeneo ya wazi ili wayachukue hadi pale yatakapohitajika," amesema Mtinangi.
Amesema wafanyabiashara wa eneo lile walipewa na muda manispaa itakapofika waondoke ili ujenzi uweze kuanza ambapo unatarajiwa kuchukua miezi sita kukamilika.
"Kwa sasa zimeshatolewa Sh500 milioni lakini ujenzi huo wa gorofa utagharimu zaidi ya Sh1 bilioni hadi kukamilika," amesema Mtinangi.
Aidha Mkurugenzi huyo amefafanua kuwa makubaliano ya Manispaa wanapotoa eneo kwa mtu pale linapohitajika wanapaswa kuondoka, hivyo kila eneo la wazi hupangishwa kwa makubaliano.
Hata hivyo, amesema Shilole aliomba eneo lingine baada ya kupewa notisi na kuelekezwa kwenda kuangalia maeneo mengine mbalimbali ilinachague sehemu inayofaa.
"Walipewa notisi ya siku 14 na Kata ya Kinondoni hawakuondoka baadae Manispaa nayo ikatoa notisi hadi wanaondoka saivi itakuwa ni zaidi ya miezi miwili," ameongeza.
Shilole amethibitisha kupokea tamko hilo na kumshukuru Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Godwin Gondwe kumuwezesha kupata eneo lingine mbadala kwa ajili ya kuendeleza biashara hiyo.