KIKOSI cha Simba, jana Jumamosi kiliondoka nchini kishua kwenda Dubai kwa ajili ya kambi ya wiki moja kujiandaa na mashindano ya Ligi Kuu Bara, Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho la Azam Sports, huku wakichimba mkwara mzito kuwa watarudi wakiwa na moto wa hatari.
Safari hiyo ni mwaliko rasmi wa Rais wa Heshima wa Simba, Mohammed Dewji kwa ajili ya kumpa muda kocha mkuu mpya wa kikosi hicho, Robert Olivieira ‘Robertinho’ kukiandaa kikosi chake, ili kikirudi, kiwe na moto.
Akizungumza na Spoti Xtra muda mfupi kabla ya kupanda ndege Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema: “Tunamshukuru Rais wetu wa heshima, Mohammed Dewji kwa mwaliko huu wa kwenda Dubai.
“Jambo hili lina mchango mkubwa kiufundi kwenye kikosi chetu ukizingatia tuna mwalimu mgeni ambaye hajapata muda wa kukaa na kikosi, hivyo kitendo cha kupata kambi ya siku saba kukaa na wachezaji inampa fursa kubwa ya kufanya tathmini kwenye kikosi chetu.
“Tuna michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi ambapo tutaanza dhidi ya Horoya mwanzoni mwa mwezi Februari, pia tukirejea tuna mchezo wa ligi dhidi ya Mbeya City, hivyo muda ni mchache, nafasi hii ya kufanya kambi ya mazoezi Dubai ni fursa kwetu kwa mashindano ambayo tunashiriki.
“Kwenye msafara huu tunawakosa Henock Inonga ambaye ni majeruhi, Nelson Okwa pamoja na Vicent Akpan kutokana na masuala ya Visa na Moses Phiri ambaye ataungana na wenzake moja kwa moja Dubai.”
Akizungumzia kambi hiyo, Kocha Msaidizi wa Simba, Juma Mgunda, alisema: “Tunaenda kwenye maandalizi tukiwa na malengo ya kuhakikisha kikosi kinarudi kikiwa na ubora mkubwa zaidi kwa ajili ya mashindano yaliyo mbele yetu.”
Ikiwa huko katika kambi yao ya kishua ambayo ina kila kitu cha kisasa kuanzia gym, bwawa la kuogelea na uwanja wa mazoezi, Simba inatarajiwa kucheza mechi mbili za kirafiki kabla ya kurudi Januari 14, mwaka huu.
STORI NA HUSSEIN MSOLEKA NA JOEL THOMAS