Simon Msuva Afichua Siri Soka Saudi Arabia



WINGA wa Al-Qadsiah ya Saudi Arabia, Mtanzania Simon Msuva, amesema ili mchezaji afanikiwe kwenye ligi ya nchini humo, analazimika kutumia nguvu na akili kwa wakati mmoja, vinginevyo ataishia kushangaa.

Msuva alitofautisha na Morocco ambako wanatumia akili na mbinu kuhakikisha timu inapata matokeo ya ushindi na kwamba nguvu siyo kitu wanachokizingatia, wakiamini mchezaji akiwa mbunifu atafanya majukumu yake kwa usahihi.

Akizungumza na Mwanaspoti, Msuva ambaye anacheza Ligi Daraja la Kwanza Saudi Arabia, alisema ligi ya huko inatumia nguvu na akili kwa wakati mmoja, akikiri sio lelemama kupata matokeo ya ushindi.

"Huku sio ajabu kufungwa na timu ndogo, tofauti na Morocco ambako timu ambazo hazina uzoefu inakuwa ngumu kupata matokeo ya kushinda, kwani wanatumia akili kubwa kucheza mechi.


"Mfano timu yetu ndio inaanza kujengwa lakini ina uwezo wa kupata matokeo na timu yoyote, hilo linamfanya mchezaji muda mwingi awe fiti akijua anacheza ligi ya nguvu, jambo ambalo kwangu naona ni sawa kwani nipo kwa ajili ya kufanya kazi ."

Alisema kwa aina ya soka hilo ni vigumu kwa mchezaji kuwa mvivu wa kufanya mazoezi kwani asipokuwa fiti hawezi kustahimili kucheza kwa mafanikio na ushindani unaotakiwa.

"Kama hauna mazoezi ya kutosha unaumbuka kweupe kwani huwezi kustahimili mikikimikiki na kuna ushindani wa namba kila mmoja anataka kuonyesha alichonacho na nilichokipenda hakuna kulazimishwa mazoezi ili ucheze utalazimika uwe na nidhamu ya kazi," alisema.

Nje na uwanja, maisha hayamsumbui kwani anawaona ni watu wenye utu kulingana na nchi hiyo kuwa ya kidini zaidi, pia alisema alipata uzoefu wa maisha ya Morocco.

"Ni watu wenye huruma nadhani inatokana na imani yao ya kidini, pia maisha ya namna hiyo siyo mageni kwangu kwa sababu niliishi Morocco,"alisema.

Timu alizopitia Msuva kabla ya kujiunga na Al-Qadsiah ni Azam FC (2010/2011), Moro United (2011/12),Yanga (2012-2017), Difaa El Jadida (2017-2020) na Wydad (2020-2022).
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad